35
Furaha Ya Waliokombolewa 
 1 Jangwa na nchi kame vitafurahi; 
nyika itashangilia na kuchanua maua. 
Kama waridi,  2 litachanua maua, 
litashangilia sana na kupaza sauti kwa furaha. 
Litapewa utukufu wa Lebanoni, 
fahari ya Karmeli na Sharoni; 
wataona utukufu wa Bwana, 
fahari ya Mungu wetu. 
 3 Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, 
yafanyeni imara magoti yaliyolegea, 
 4 waambieni wale wenye mioyo ya hofu, 
“Kuweni hodari, msiogope; 
tazama, Mungu wenu atakuja, 
pamoja na malipo ya Mungu, 
atakuja na kuwaokoa ninyi.” 
 5 Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa 
na masikio ya viziwi yatazibuliwa. 
 6 Ndipo kilema atarukaruka kama kulungu, 
nao ulimi wa aliye bubu utapaza sauti kwa shangwe. 
Maji yatatiririka kwa kasi katika nyika, 
na vijito katika jangwa. 
 7 Mchanga wa moto utakuwa bwawa la maji, 
ardhi yenye kiu itabubujika chemchemi. 
Maskani ya mbweha walikolala hapo awali 
patamea majani, matete na mafunjo. 
 8 Nako kutakuwa na njia kuu, 
nayo itaitwa Njia ya Utakatifu. 
Wasio safi hawatapita juu yake; 
itakuwa ya wale watembeao katika Njia ile; 
yeye asafiriye juu yake, 
ajapokuwa mjinga, hatapotea. 
 9 Huko hakutakuwepo na simba, 
wala mnyama mkali hatapita njia hiyo, 
wala hawatapatikana humo. 
Ila waliokombolewa tu ndio watakaopita huko, 
 10 waliokombolewa na Bwana watarudi. 
Wataingia Sayuni wakiimba; 
furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao. 
Watapata furaha na shangwe; 
huzuni na majonzi vitakimbia.