55
Mwaliko Kwa Wenye Kiu 
 1 “Njooni, ninyi nyote wenye kiu, 
njooni kwenye maji; 
nanyi ambao hamna fedha, 
njooni, nunueni na mle! 
Njooni, nunueni divai na maziwa 
bila fedha na bila gharama. 
 2 Kwa nini kutumia fedha kwa kitu ambacho si chakula, 
na kutaabikia kitu kisichoshibisha? 
Sikilizeni, nisikilizeni mimi na mle kilicho kizuri, 
nazo nafsi zenu zitafurahia utajiri wa unono. 
 3 Tegeni sikio mje kwangu, 
nisikieni mimi, ili nafsi zenu zipate kuishi. 
Nitafanya agano la milele nanyi, 
pendo la uaminifu nililomwahidi Daudi. 
 4 Tazama, nimemfanya kuwa shahidi wa mataifa, 
kiongozi na jemadari wa mataifa. 
 5 Hakika utaita mataifa usiyoyajua, 
nayo mataifa yale yasiyokujua yataharakisha kukujia, 
kwa sababu ya Bwana Mungu wako, 
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, 
kwa maana amekutukuza.” 
 6 Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana; 
mwiteni maadamu yu karibu. 
 7 Mtu mwovu na aiache njia yake, 
na mtu mbaya na ayaache mawazo yake. 
Yeye na amrudie Bwana, naye atamrehemu, 
arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa. 
 8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu, 
wala njia zenu si njia zangu,” 
asema Bwana. 
 9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia, 
ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu 
na mawazo yangu kuliko mawazo yenu. 
 10 Kama vile mvua na theluji 
ishukavyo kutoka mbinguni, 
nayo hairudi tena huko 
bila kunywesha dunia 
na kuichipusha na kuistawisha, 
hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi 
na mkate kwa mlaji, 
 11 ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu: 
Halitanirudia tupu, 
bali litatimiliza lile nililokusudia 
na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma. 
 12 Mtatoka nje kwa furaha 
na kuongozwa kwa amani; 
milima na vilima 
vitapaza sauti kwa nyimbo mbele yenu, 
nayo miti yote ya shambani 
itapiga makofi. 
 13 Badala ya kichaka cha miiba 
itaota miti ya misunobari, 
na badala ya michongoma 
Hili litakuwa jambo la kumpatia Bwana jina, 
kwa ajili ya ishara ya milele, 
ambayo haitaharibiwa.”