Yoeli  
 1
 1 Neno la Bwana ambalo lilimjia Yoeli mwana wa Pethueli. 
Uvamizi Wa Nzige 
 2 Sikilizeni hili, enyi wazee; 
sikilizeni, ninyi nyote mnaoishi katika nchi. 
Je, jambo kama hili lilishawahi kutokea 
katika siku zenu au katika siku za babu zenu? 
 3 Waelezeni watoto wenu, 
na watoto wenu wawaambie watoto wao, 
na watoto wao kwa kizazi kitakachofuata. 
 4 Kilichosazwa na kundi la tunutu 
nzige wakubwa wamekula, 
kilichosazwa na nzige wakubwa 
parare wamekula, 
kilichosazwa na parare 
madumadu wamekula. 
 5 Amkeni, enyi walevi, mlie! 
Pigeni yowe enyi wanywaji wote wa mvinyo, 
pigeni yowe kwa sababu ya mvinyo mpya, 
kwa kuwa mmenyangʼanywa 
kutoka midomoni mwenu. 
 6 Taifa limevamia nchi yangu, 
lenye nguvu tena lisilo na idadi; 
lina meno ya simba, 
magego ya simba jike. 
 7 Limeharibu mizabibu yangu 
na kuangamiza mitini yangu. 
Limebambua magome yake 
na kuyatupilia mbali, 
likayaacha matawi yake yakiwa meupe. 
 8 Omboleza kama bikira aliyevaa nguo ya gunia 
anayehuzunika kwa ajili ya mume wa ujana wake. 
 9 Sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji 
zimekatiliwa mbali kutoka nyumba ya Bwana. 
Makuhani wanaomboleza, 
wale wanaohudumu mbele za Bwana. 
 10 Mashamba yameharibiwa, 
ardhi imekauka; 
nafaka imeharibiwa, 
mvinyo mpya umekauka, 
mafuta yamekoma. 
 11 Kateni tamaa, enyi wakulima, 
lieni, enyi mlimao mizabibu; 
huzunikeni kwa ajili ya ngano na shayiri, 
kwa sababu mavuno ya shambani yameharibiwa. 
 12 Mzabibu umekauka 
na mtini umenyauka; 
mkomamanga, mtende na mtofaa, 
miti yote shambani, imekauka. 
Hakika furaha yote ya mwanadamu 
imeondoka. 
Wito Wa Toba 
 13 Vaeni nguo ya gunia, enyi makuhani, muomboleze; 
pigeni yowe, enyi mnaohudumu madhabahuni. 
Njooni, vaeni nguo ya gunia usiku kucha, 
enyi mnaohudumu mbele za Mungu wangu; 
kwa kuwa sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji 
zimezuiliwa kufika katika nyumba ya Mungu wenu. 
 14 Tangazeni saumu takatifu; 
liiteni kusanyiko takatifu. 
Iteni wazee 
na wote waishio katika nchi 
waende katika nyumba ya Bwana Mungu wenu, 
wakamlilie Bwana. 
 15 Ole kwa siku hiyo! 
Kwa kuwa siku ya Bwana iko karibu; 
itakuja kama uharibifu 
kutoka kwa Mwenyezi.* Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania. 
 16 Je, chakula hakikukatiliwa mbali 
mbele ya macho yetu: 
furaha na shangwe 
kutoka nyumba ya Mungu wetu? 
 17 Mbegu zinakauka 
chini ya mabonge ya udongo. 
Ghala zimeachwa katika uharibifu, 
ghala za nafaka zimebomolewa, 
kwa maana hakuna nafaka. 
 18 Jinsi gani ngʼombe wanavyolia! 
Makundi ya mifugo yanahangaika 
kwa sababu hawana malisho; 
hata makundi ya kondoo yanateseka. 
 19 Kwako, Ee Bwana, naita, 
kwa kuwa moto umeteketeza 
malisho ya mbugani 
na miali ya moto imeunguza 
miti yote shambani. 
 20 Hata wanyama wa porini wanakuonea shauku; 
vijito vya maji vimekauka, 
na moto umeteketeza 
malisho yote ya mbugani.