5
Mtawala Aliyeahidiwa Kutoka Bethlehemu 
 1 Panga majeshi yako, ee mji wa majeshi, 
kwa kuwa kuzingirwa kumepangwa dhidi yetu. 
Watampiga mtawala wa Israeli 
shavuni kwa fimbo. 
 2 “Lakini wewe, Bethlehemu Efrathi, 
ingawa u mdogo miongoni mwa koo za Yuda, 
kutoka kwako atatokea kwa ajili yangu 
yeye atakayekuwa mtawala katika Israeli, 
ambaye asili yake ni kutoka zamani, 
kutoka milele.” 
 3 Kwa hiyo Israeli utaachwa mpaka wakati 
mwanamke aliye na utungu atakapozaa 
na ndugu zake wengine warudi 
kujiunga na Waisraeli. 
 4 Atasimama na kulichunga kundi lake 
katika nguvu ya Bwana, 
katika utukufu wa jina la Bwana Mungu wake. 
Nao wataishi kwa usalama, kwa kuwa wakati huo 
ukuu wake utaenea hadi miisho ya dunia. 
 5 Naye atakuwa amani yao. 
Ukombozi Na Uharibifu 
Wakati Mwashuru atakapovamia nchi yetu 
na kupita katika ngome zetu, 
tutawainua wachungaji saba dhidi yake, 
hata viongozi wanane wa watu. 
 6 Wataitawala nchi ya Ashuru kwa upanga, 
nchi ya Nimrodi kwa upanga. 
Atatuokoa kutoka kwa Mwashuru 
atakapoivamia nchi yetu 
na kuingia katika mipaka yetu. 
 7 Mabaki ya Yakobo yatakuwa 
katikati ya mataifa mengi 
kama umande kutoka kwa Bwana, 
kama manyunyu juu ya majani, 
ambayo hayamngoji mtu 
wala kukawia kwa mwanadamu. 
 8 Mabaki ya Yakobo yatakuwa miongoni mwa mataifa, 
katikati ya mataifa mengi, 
kama simba miongoni mwa wanyama wa msituni, 
kama mwana simba miongoni 
mwa makundi ya kondoo, 
ambaye anaumiza vibaya na kuwararua 
kila anapopita katikati yao, 
wala hakuna awezaye kuokoa. 
 9 Mkono wako utainuliwa juu kwa ushindi juu ya watesi wako, 
nao adui zako wote wataangamizwa. 
 10 “Katika siku ile,” asema Bwana, 
“nitaangamiza farasi zenu katikati yenu 
na kubomoa magari yenu ya vita. 
 11 Nitaiangamiza miji ya nchi yenu 
na kuziangusha chini ngome zenu zote. 
 12 Nitaangamiza uchawi wenu 
na hamtapiga tena ramli. 
 13 Nitaangamiza vinyago vyenu vya kuchonga 
na mawe yenu ya ibada yatoke katikati yenu; 
hamtasujudia tena 
kazi ya mikono yenu. 
 14 Nitangʼoa nguzo za Ashera katikati yenu 
na kubomoa miji yenu. 
 15 Nitalipiza kisasi kwa hasira na ghadhabu 
juu ya mataifa ambayo hayajanitii.”