Zaburi 3
Sala Ya Asubuhi Ya Kuomba Msaada 
Zaburi ya Daudi. Alipomkimbia mwanawe Absalomu. 
 1 Ee Bwana, tazama adui zangu walivyo wengi! 
Ni wengi kiasi gani wanaoinuka dhidi yangu! 
 2 Wengi wanasema juu yangu, 
“Mungu hatamwokoa.” 
 3 Lakini wewe, Ee Bwana, ni ngao pande zote; 
umeniwekea utukufu na kuinua kichwa changu. 
 4 Ninamlilia Bwana kwa sauti kuu, 
naye ananijibu kutoka mlima wake mtakatifu. 
 5 Ninajilaza na kupata usingizi; 
naamka tena, kwa maana Bwana hunitegemeza. 
 6 Sitaogopa makumi elfu ya adui, 
wanaojipanga dhidi yangu kila upande. 
 7 Ee Bwana, amka! 
Niokoe, Ee Mungu wangu! 
Wapige adui zangu wote kwenye taya, 
vunja meno ya waovu. 
 8 Kwa maana wokovu watoka kwa Bwana. 
Baraka yako na iwe juu ya watu wako.