Zaburi 6
Sala Kwa Ajili Ya Msaada Wakati Wa Taabu 
Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Mtindo wa sheminithi.* Sheminithi ni mtajo mmojawapo katika lugha ya uimbaji. Zaburi ya Daudi. 
 1 Ee Bwana, usinikemee katika hasira yako, 
wala usiniadhibu katika ghadhabu yako. 
 2 Unirehemu Bwana, 
kwa maana nimedhoofika; 
Ee Bwana, uniponye, 
kwa maana mifupa yangu 
ina maumivu makali. 
 3 Nafsi yangu ina uchungu mwingi. 
Mpaka lini, Ee Bwana, mpaka lini? 
 4 Geuka Ee Bwana, unikomboe, 
uniokoe kwa sababu ya fadhili zako. 
 5 Hakuna mtu anayekukumbuka 
akiwa amekufa. 
Ni nani awezaye kukusifu 
akiwa kuzimu? 
 6 Nimechakaa kwa kulia kwa huzuni; 
usiku kucha nafurikisha 
kitanda changu kwa machozi; 
nimelowesha viti vyangu vya fahari 
kwa machozi. 
 7 Macho yangu yamedhoofika kwa kuhuzunika, 
yamedhoofika kwa sababu ya adui zangu wote. 
 8 Kaeni mbali nami, ninyi nyote mtendao mabaya, 
kwa maana Bwana amesikia kulia kwangu. 
 9  Bwana amesikia kilio changu kwa huruma, 
Bwana amekubali sala yangu. 
 10 Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, 
watarudi nyuma kwa aibu ya ghafula.