Zaburi 8
Utukufu Wa Mungu Na Heshima Ya Mwanadamu 
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya Daudi. 
 1 Ee Bwana, Bwana wetu, 
tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! 
Umeuweka utukufu wako 
juu ya mbingu. 
 2 Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao 
umeamuru sifa, 
kwa sababu ya watesi wako, 
kumnyamazisha adui na mlipiza kisasi. 
 3 Nikiziangalia mbingu zako, 
kazi ya vidole vyako, 
mwezi na nyota, 
ulizoziratibisha, 
 4 mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria, 
binadamu ni nani hata unamjali? 
 5 Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni, 
ukamvika taji ya utukufu na heshima. 
 6 Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako; 
umeweka vitu vyote chini ya miguu yake. 
 7 Mifugo na makundi yote pia, 
naam, na wanyama wa kondeni, 
 8 ndege wa angani na samaki wa baharini, 
naam, kila kiogeleacho katika njia za bahari. 
 9 Ee Bwana, Bwana wetu, 
tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!