Zaburi 20
Maombi Kwa Ajili Ya Ushindi 
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. 
 1  Bwana na akujibu unapokuwa katika dhiki, 
jina la Mungu wa Yakobo na liwe kinga yako. 
 2 Na akutumie msaada kutoka patakatifu 
na akupatie msaada kutoka Sayuni. 
 3 Na azikumbuke dhabihu zako zote, 
na azikubali sadaka zako za kuteketezwa. 
 4 Na akujalie haja ya moyo wako, 
na aifanikishe mipango yako yote. 
 5 Tutashangilia kwa furaha utakaposhinda, 
tutainua bendera zetu kwa jina la Mungu wetu. 
Bwana na akupe haja zako zote. 
 6 Sasa nafahamu kuwa Bwana 
humwokoa mpakwa mafuta wake, 
humjibu kutoka mbingu yake takatifu 
kwa nguvu za wokovu wa mkono wake wa kuume. 
 7 Wengine wanatumaini magari ya vita, na wengine farasi, 
bali sisi tutalitumainia jina la Bwana, Mungu wetu. 
 8 Wao wameshushwa chini na kuanguka, 
bali sisi tunainuka na kusimama imara. 
 9 Ee Bwana, mwokoe mfalme! 
Tujibu tunapokuita!