Zaburi 32
Furaha Ya Msamaha 
Zaburi ya Daudi. Funzo. 
 1 Heri mtu yule ambaye amesamehewa makosa yake, 
ambaye dhambi zake zimefunikwa. 
 2 Heri mtu yule ambaye Bwana 
hamhesabii dhambi, 
na ambaye rohoni mwake 
hamna udanganyifu. 
 3 Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa 
kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa. 
 4 Usiku na mchana 
mkono wako ulinilemea, 
nguvu zangu zilinyonywa 
kama vile katika joto la kiangazi. 
 5 Kisha nilikujulisha dhambi yangu 
wala sikuficha uovu wangu. 
Nilisema, “Nitaungama 
makosa yangu kwa Bwana.” 
Ndipo uliponisamehe 
hatia ya dhambi yangu. 
 6 Kwa hiyo kila mtu mcha Mungu akuombe 
wakati unapopatikana, 
hakika maji makuu yatakapofurika 
hayatamfikia yeye. 
 7 Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha, 
utaniepusha na taabu 
na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu. 
 8 Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; 
nitakushauri na kukuangalia. 
 9 Usiwe kama farasi au nyumbu 
wasio na akili, 
ambao ni lazima waongozwe kwa lijamu na hatamu 
la sivyo hawatakukaribia. 
 10 Mtu mwovu ana taabu nyingi, 
bali upendo usio na kikomo wa Bwana 
unamzunguka mtu anayemtumaini. 
 11 Shangilieni katika Bwana na mfurahi, enyi wenye haki! 
Imbeni, nyote mlio wanyofu wa moyo!