Zaburi 38
Maombi Ya Mtu Anayeteseka 
Zaburi ya Daudi. Maombi. 
 1 Ee Bwana, usinikemee katika hasira yako, 
wala kuniadhibu katika ghadhabu yako. 
 2 Kwa kuwa mishale yako imenichoma, 
na mkono wako umenishukia. 
 3 Hakuna afya mwilini mwangu 
kwa sababu ya ghadhabu yako, 
mifupa yangu haina uzima 
kwa sababu ya dhambi zangu. 
 4 Maovu yangu yamenifunika 
kama mzigo usiochukulika. 
 5 Majeraha yangu yameoza na yananuka, 
kwa sababu ya upumbavu wa dhambi zangu. 
 6 Nimeinamishwa chini na kushushwa sana, 
mchana kutwa nazunguka nikiomboleza. 
 7 Viuno vyangu vimejaa maumivu yaunguzayo, 
hakuna afya mwilini mwangu. 
 8 Nimedhoofika na kupondwa kabisa, 
nasononeka kwa maumivu makuu ya moyoni. 
 9 Ee Bwana, yote ninayoyaonea shauku 
yako wazi mbele zako, 
kutamani kwangu sana 
hakufichiki mbele zako. 
 10 Moyo wangu unapigapiga, 
nguvu zangu zimeniishia; 
hata macho yangu yametiwa giza. 
 11 Rafiki na wenzangu wananikwepa 
kwa sababu ya majeraha yangu; 
majirani zangu wanakaa mbali nami. 
 12 Wale wanaotafuta uhai wangu 
wanatega mitego yao, 
wale ambao wangetaka kunidhuru 
huongea juu ya maangamizi yangu; 
hufanya shauri la hila mchana kutwa. 
 13 Mimi ni kama mtu kiziwi, asiyeweza kusikia, 
ni kama bubu, asiyeweza kufungua kinywa chake, 
 14 nimekuwa kama mtu asiyesikia, 
ambaye kinywa chake hakiwezi kutoa jibu. 
 15 Ee Bwana, ninakungojea wewe, 
Ee Bwana Mungu wangu, utajibu. 
 16 Kwa kuwa nilisema, “Usiwaache wafurahie, 
wala wasijitukuze juu yangu 
mguu wangu unapoteleza.” 
 17 Kwa maana ninakaribia kuanguka, 
na maumivu yangu yananiandama siku zote. 
 18 Naungama uovu wangu, 
ninataabishwa na dhambi yangu. 
 19 Wengi ni wale ambao ni adui zangu hodari, 
wale wanaonichukia bila sababu ni wengi. 
 20 Wanaolipa maovu kwa wema wangu 
hunisingizia ninapofuata lililo jema. 
 21 Ee Bwana, usiniache, 
usiwe mbali nami, Ee Mungu wangu. 
 22 Ee Bwana Mwokozi wangu, 
uje upesi kunisaidia.