Zaburi 43
Maombi Ya Mtu Aliyeko Uhamishoni Yanaendelea 
 1 Ee Mungu unihukumu, 
nitetee dhidi ya taifa lisilomcha Mungu, 
niokoe na watu wadanganyifu na waovu. 
 2 Wewe ni Mungu ngome yangu. 
Kwa nini umenikataa? 
Kwa nini niendelee kuomboleza, 
nikiwa nimeonewa na adui? 
 3 Tuma hima nuru yako na kweli yako 
na viniongoze; 
vinilete mpaka mlima wako mtakatifu, 
mpaka mahali unapoishi. 
 4 Ndipo nitakwenda madhabahuni pa Mungu, 
kwa Mungu, furaha yangu na shangwe yangu. 
Nitakusifu kwa kinubi, 
Ee Mungu, Mungu wangu. 
 5 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka? 
Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu? 
Weka tumaini lako kwa Mungu, 
kwa sababu bado nitamsifu 
Mwokozi wangu na Mungu wangu.