Zaburi 46
Mungu Yuko Pamoja Nasi 
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi. 
 1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, 
msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. 
 2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa 
nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari. 
 3 Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka, 
milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake. 
 4 Kuna mto ambao vijito vyake vinaufurahisha mji wa Mungu, 
mahali patakatifu ambako Aliye Juu Sana anaishi. 
 5 Mungu yuko katikati yake, hautaanguka, 
Mungu atausaidia asubuhi na mapema. 
 6 Mataifa yanafanya ghasia, falme zinaanguka, 
Yeye huinua sauti yake, dunia ikayeyuka. 
 7  Bwana Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi, 
Mungu wa Yakobo ni ngome yetu. 
 8 Njooni mkaone kazi za Bwana 
jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi. 
 9 Anakomesha vita hata miisho ya dunia, 
anakata upinde na kuvunjavunja mkuki, 
anateketeza ngao kwa moto. 
 10 “Tulieni, mjue ya kwamba mimi ndimi Mungu; 
nitatukuzwa katikati ya mataifa, 
nitatukuzwa katika dunia.” 
 11  Bwana Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi; 
Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.