Zaburi 70
Kuomba Msaada 
(Zaburi 40:13-17) 
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Maombi. 
 1 Ee Mungu, ufanye haraka kuniokoa; 
Ee Bwana, njoo hima unisaidie. 
 2 Wale wanaotafuta kuuondoa uhai wangu, 
waaibishwe na kufadhaishwa; 
wote wanaotamani kuangamizwa kwangu, 
warudishwe nyuma kwa aibu. 
 3 Wale waniambiao, “Aha! Aha!” 
warudi nyuma kwa sababu ya aibu yao. 
 4 Lakini wote wakutafutao 
washangilie na kukufurahia, 
wale wapendao wokovu wako siku zote waseme, 
“Mungu na atukuzwe!” 
 5 Lakini bado mimi ni maskini na mhitaji; 
Ee Mungu, unijie haraka. 
Wewe ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu; 
Ee Bwana, usikawie.