Zaburi 79
Maombi Kwa Ajili Ya Wokovu Wa Taifa 
Zaburi ya Asafu. 
 1 Ee Mungu, mataifa yameuvamia urithi wako, 
wamelinajisi Hekalu lako takatifu, 
wameifanya Yerusalemu kuwa magofu. 
 2 Wametoa maiti za watumishi 
kuwa chakula cha ndege wa angani 
na nyama ya watakatifu wako 
kwa wanyama wa nchi. 
 3 Wamemwaga damu kama maji 
kuzunguka Yerusalemu yote, 
wala hakuna yeyote wa kuwazika. 
 4 Tumekuwa kitu cha aibu kwa jirani zetu, 
cha dharau na mzaha kwa wale wanaotuzunguka. 
 5 Hata lini, Ee Bwana? Je, wewe utakasirika milele? 
Wivu wako utawaka kama moto hadi lini? 
 6 Mwaga ghadhabu yako kwa mataifa yasiyokukubali, 
juu ya falme za hao wasioliitia jina lako, 
 7 kwa maana wamemrarua Yakobo 
na kuharibu nchi ya makao yake. 
 8 Usituhesabie dhambi za baba zetu, 
huruma yako na itujie hima, 
kwa maana tu wahitaji mno. 
 9 Ee Mungu Mwokozi wetu, utusaidie, 
kwa ajili ya utukufu wa jina lako; 
tuokoe na kutusamehe dhambi zetu 
kwa ajili ya jina lako. 
 10 Kwa nini mataifa waseme, 
“Yuko wapi Mungu wenu?” 
Mbele ya macho yetu, 
dhihirisha kati ya mataifa 
kwamba unalipiza kisasi damu iliyomwagwa 
ya watumishi wako. 
 11 Kilio cha huzuni cha wafungwa kifike mbele zako; 
kwa nguvu za mkono wako 
hifadhi wale waliohukumiwa kufa. 
 12 Walipize jirani zetu mara saba vifuani mwao 
aibu walizovurumisha juu yako, Ee Bwana. 
 13 Ndipo sisi watu wako, kondoo wa malisho yako, 
tutakusifu milele; 
toka kizazi hadi kizazi 
tutasimulia sifa zako.