Zaburi 82
Maombi Kwa Ajili Ya Kutaka Haki 
Zaburi ya Asafu. 
 1 Mungu anaongoza kusanyiko kuu, 
anatoa hukumu miongoni mwa “miungu”: 
 2 “Hata lini utaendelea kuwatetea wasio haki 
na kuonyesha upendeleo kwa waovu? 
 3 Teteeni wanyonge na yatima, 
tunzeni haki za maskini na walioonewa. 
 4 Mwokoeni mnyonge na mhitaji, 
wakomboeni kutoka mkononi mwa mwovu. 
 5 “Hawajui lolote, hawaelewi lolote. 
Wanatembea gizani; 
misingi yote ya dunia imetikisika. 
 6 “Nilisema, ‘Ninyi ni “miungu”; 
ninyi nyote ni wana wa Aliye Juu Sana.’ 
 7 Lakini mtakufa kama wanadamu wa kawaida; 
mtaanguka kama mtawala mwingine yeyote.” 
 8 Ee Mungu, inuka uihukumu nchi, 
kwa kuwa mataifa yote ni urithi wako.