Zaburi 84
Kuionea Shauku Nyumba Ya Mungu 
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya wana wa Kora. 
 1 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, 
makao yako yapendeza kama nini! 
 2 Nafsi yangu inatamani sana, 
naam, hata kuona shauku, 
kwa ajili ya nyua za Bwana; 
moyo wangu na mwili wangu 
vinamlilia Mungu Aliye Hai. 
 3 Hata shomoro amejipatia makao, 
mbayuwayu amejipatia kiota 
mahali awezapo kuweka makinda yake: 
mahali karibu na madhabahu yako, 
Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, 
Mfalme wangu na Mungu wangu. 
 4 Heri wale wanaokaa nyumbani mwako, 
wanaokusifu wewe daima. 
 5 Heri wale ambao nguvu zao ziko kwako, 
na njia ziendazo Sayuni zimo mioyoni mwao. 
 6 Wanapopita katika Bonde la Baka,* Yaani Bonde la Vilio. 
hulifanya mahali pa chemchemi, 
pia mvua za vuli hulijaza kwa madimbwi.† Au: baraka. 
 7 Huendelea toka nguvu hadi nguvu, 
hadi kila mmoja afikapo 
mbele za Mungu huko Sayuni. 
 8 Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, sikia maombi yangu; 
nisikilize, Ee Mungu wa Yakobo. 
 9 Ee Mungu, uitazame ngao yetu, 
mtazame kwa wema mpakwa mafuta wako. 
 10 Siku moja katika nyua zako ni bora 
kuliko siku elfu mahali pengine; 
afadhali ningekuwa bawabu katika nyumba ya Mungu wangu 
kuliko kukaa katika mahema ya waovu. 
 11 Kwa kuwa Bwana ni jua na ngao, 
Bwana hutoa wema na heshima; 
hakuna kitu chema anachowanyima 
wale ambao hawana hatia. 
 12 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, 
heri ni mtu yule anayekutumaini wewe.