Zaburi 96
Mungu Mfalme Mkuu 
(1 Nyakati 16:23-33) 
 1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya; 
mwimbieni Bwana dunia yote. 
 2 Mwimbieni Bwana, lisifuni jina lake; 
tangazeni wokovu wake siku baada ya siku. 
 3 Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa, 
matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote. 
 4 Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote; 
yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote. 
 5 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, 
lakini Bwana aliziumba mbingu. 
 6 Fahari na enzi viko mbele yake; 
nguvu na utukufu vimo patakatifu pake. 
 7 Mpeni Bwana, enyi jamaa za mataifa, 
mpeni Bwana utukufu na nguvu. 
 8 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake; 
leteni sadaka na mje katika nyua zake. 
 9 Mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake; 
dunia yote na itetemeke mbele zake. 
 10 Katikati ya mataifa semeni, “Bwana anatawala.” 
Ulimwengu ameuweka imara, hauwezi kusogezwa; 
atawahukumu watu kwa uadilifu. 
 11 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi; 
bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake; 
 12 mashamba na yashangilie, 
pamoja na vyote vilivyomo ndani yake. 
Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha; 
 13 itaimba mbele za Bwana kwa maana anakuja, 
anakuja kuihukumu dunia. 
Ataihukumu dunia kwa haki, 
na mataifa katika kweli yake.