Zaburi 144
Mfalme Amshukuru Mungu Kwa Ushindi 
Zaburi ya Daudi. 
 1 Sifa ni kwa Bwana Mwamba wangu, 
aifundishaye mikono yangu vita, 
na vidole vyangu kupigana. 
 2 Yeye ni Mungu wangu wa upendo na boma langu, 
ngome yangu na mwokozi wangu, 
ngao yangu ninayemkimbilia, 
ambaye huwatiisha mataifa chini yangu. 
 3 Ee Bwana, mwanadamu ni nini hata umjali, 
Binadamu ni nini hata umfikirie? 
 4 Mwanadamu ni kama pumzi, 
siku zake ni kama kivuli kinachopita. 
 5 Ee Bwana, pasua mbingu zako, ushuke, 
gusa milima ili itoe moshi. 
 6 Peleka umeme uwatawanye adui, 
lenga mishale yako uwashinde. 
 7 Nyoosha mkono wako kutoka juu, 
nikomboe na kuniokoa 
kutoka maji makuu, 
kutoka mikononi mwa wageni 
 8 ambao vinywa vyao vimejaa uongo, 
na mikono yao ya kuume ni midanganyifu. 
 9 Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya, 
kwa zeze yenye nyuzi kumi nitakuimbia, 
 10 kwa Yule awapaye wafalme ushindi, 
ambaye humwokoa Daudi, mtumishi wake kutokana na upanga hatari. 
 11 Nikomboe na uniokoe 
kutoka mikononi mwa wageni 
ambao vinywa vyao vimejaa uongo, 
na mikono yao ya kuume ni midanganyifu. 
 12 Kisha wana wetu wakati wa ujana wao 
watakuwa kama mimea iliyotunzwa vizuri, 
binti zetu watakuwa kama nguzo zilizoviringwa 
kurembesha jumba la kifalme. 
 13 Ghala zetu zitajazwa 
aina zote za mahitaji. 
Kondoo zetu watazaa kwa maelfu, 
kwa makumi ya maelfu katika mashamba yetu; 
 14 maksai wetu watakokota 
mizigo mizito. 
Hakutakuwa na kubomoka kuta, 
hakuna kuchukuliwa mateka, 
wala kilio cha taabu 
katika barabara zetu. 
 15 Heri watu ambao hili ni kweli; 
heri wale ambao Bwana ni Mungu wao.