Zaburi 149
Wimbo Wa Kumsifu Mungu Kwa Wema Wake 
 1 Msifuni Bwana. 
Mwimbieni Bwana wimbo mpya, 
sifa zake katika kusanyiko la watakatifu. 
 2 Israeli na washangilie katika Muumba wao, 
watu wa Sayuni na wafurahi katika Mfalme wao. 
 3 Na walisifu jina lake kwa kucheza 
na wampigie muziki kwa matari na kinubi. 
 4 Kwa maana Bwana anapendezwa na watu wake, 
anawavika wanyenyekevu taji ya wokovu. 
 5 Watakatifu washangilie katika heshima hii, 
na waimbe kwa shangwe vitandani mwao. 
 6 Sifa za Mungu na ziwe vinywani mwao 
na upanga ukatao kuwili mikononi mwao, 
 7 ili walipize mataifa kisasi 
na adhabu juu ya mataifa, 
 8 wawafunge wafalme wao kwa minyororo, 
wakuu wao kwa pingu za chuma, 
 9 ili kuwafanyia hukumu iliyoandikwa dhidi yao. 
Huu ndio utukufu wa watakatifu wake wote. 
Msifuni Bwana.