8
 1 Laiti ungelikuwa kwangu kama ndugu wa kiume, 
ambaye aliyanyonya matiti ya mama yangu! 
Kisha, kama ningekukuta huko nje, 
ningelikubusu, 
wala hakuna mtu yeyote angelinidharau. 
 2 Ningelikuongoza na kukuleta 
katika nyumba ya mama yangu, 
yeye ambaye amenifundisha. 
Ningelikupa divai iliyokolezwa unywe, 
asali ya maua ya mikomamanga yangu. 
 3 Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, 
na mkono wake wa kuume unanikumbatia. 
 4 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza: 
msichochee wala kuamsha mapenzi 
hata yatakapotaka yenyewe. 
Shairi La Sita 
Marafiki 
 5 Ni nani huyu anayekuja kutoka nyikani 
akimwegemea mpenzi wake? 
Mpendwa 
Nilikuamsha chini ya mtofaa, 
huko mama yako alipotunga mimba yako, 
huko yeye alipata utungu akakuzaa. 
 6 Nitie kama muhuri moyoni mwako, 
kama muhuri kwenye mkono wako; 
kwa maana upendo una nguvu kama mauti, 
wivu wake ni mkatili kama kuzimu. 
Unachoma kama mwali wa moto, 
kama mwali mkubwa wa moto wa Bwana hasa. 
 7 Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, 
mito haiwezi kuugharikisha. 
Kama mtu angelitoa mali yote ya nyumbani mwake 
kwa ajili ya upendo, 
angelidharauliwa kabisa. 
Marafiki 
 8 Tunaye dada mdogo, 
matiti yake hayajakua bado. 
Tutafanya nini kwa ajili ya dada yetu 
wakati atakapokuja kuposwa? 
 9 Kama yeye ni ukuta, 
tutajenga minara ya fedha juu yake. 
Na kama yeye ni mlango, 
tutamzungushia mbao za mierezi. 
Mpendwa 
 10 Mimi ni ukuta, 
nayo matiti yangu ni kama minara. 
Ndivyo ambavyo nimekuwa machoni pake 
kama yule anayeleta utoshelevu. 
 11 Solomoni alikuwa na shamba la mizabibu huko Baal-Hamoni; 
alikodisha shamba lake la mizabibu kwa wapangaji. 
Kila mmoja angeleta kwa ajili ya matunda yake 
shekeli 1,000* Shekeli 1,000 ni kama kilo 11.5. za fedha. 
 12 Lakini shamba langu la mizabibu 
ambalo ni langu mwenyewe 
ni langu kutoa; 
hizo shekeli 1,000 ni kwa ajili yako, ee Solomoni, 
na shekeli mia mbili† Shekeli 200 ni kama kilo 2.3. ni kwa ajili 
ya wale wanaotunza matunda yake. 
Mpenzi 
 13 Wewe ukaaye bustanini 
pamoja na marafiki mliohudhuria, 
hebu nisikie sauti yako! 
Mpendwa 
 14 Njoo, mpenzi wangu, 
uwe kama swala 
au kama ayala kijana 
juu ya milima iliyojaa vikolezo.