19
Maombolezo Kwa Ajili Ya Wakuu Wa Israeli 
 1 “Wewe fanya maombolezo kuhusu wakuu wa Israeli  2 na useme: 
“ ‘Tazama jinsi gani mama yako alivyokuwa simba jike 
miongoni mwa simba! 
Alilala katikati ya wana simba 
na kulisha watoto wake. 
 3 Alimlea mmoja wa watoto wake, 
naye akawa simba mwenye nguvu. 
Akajifunza kurarua mawindo 
naye akala watu. 
 4 Mataifa wakasikia habari zake, 
naye akanaswa katika shimo lao. 
Wakamwongoza kwa ndoana 
mpaka nchi ya Misri. 
 5 “ ‘Mama yake alipongoja na kuona tumaini lake halitimiziki, 
nayo matarajio yake yametoweka, 
akamchukua mwanawe mwingine 
na kumfanya simba mwenye nguvu. 
 6 Alizungukazunguka miongoni mwa simba, 
kwa kuwa sasa alikuwa simba mwenye nguvu. 
Akajifunza kurarua mawindo 
naye akala watu. 
 7 Akabomoa ngome zao 
na kuiharibu miji yao. 
Nchi na wote waliokuwa ndani yake 
wakatiwa hofu kwa kunguruma kwake. 
 8 Kisha mataifa wakaja dhidi yake 
kutoka sehemu zilizomzunguka. 
Wakatanda nyavu zao kwa ajili yake, 
naye akanaswa katika shimo lao. 
 9 Kwa kutumia ndoana wakamvutia kwenye tundu 
na kumleta mpaka kwa mfalme wa Babeli. 
Wakamtia gerezani, hivyo kunguruma kwake 
hakukusikika tena 
katika milima ya Israeli. 
 10 “ ‘Mama yako alikuwa kama mzabibu 
katika shamba lako la mizabibu 
uliopandwa kando ya maji, 
ukiwa unazaa sana na wenye matawi mengi 
kwa sababu ya wingi wa maji. 
 11 Matawi yake yalikuwa na nguvu, 
yaliyofaa kuwa fimbo ya enzi ya mtawala. 
Ulikuwa mrefu kupita miti mingine 
katikati ya matawi manene; 
ulionekana kwa urahisi 
kwa ajili ya urefu wake 
na wingi wa matawi yake. 
 12 Lakini ulingʼolewa kwa hasira kali 
na kutupwa chini. 
Upepo wa mashariki uliufanya usinyae, 
matunda yake yakapukutika, 
matawi yake yenye nguvu yakanyauka 
na moto ukayateketeza. 
 13 Sasa umepandwa jangwani 
katika nchi kame na ya kiu. 
 14 Moto ulienea kuanzia katika mmojawapo ya matawi yake makubwa 
na kuteketeza matunda yake. 
Hakuna tawi lenye nguvu lililobaki juu yake 
lifaalo kuwa fimbo ya enzi ya mtawala.’ 
Hili ndilo ombolezo, na litumike kama ombolezo.”