27
Maombolezo Kwa Ajili Ya Tiro 
 1 Neno la Bwana likanijia kusema:  2 “Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Tiro.  3 Umwambie Tiro, ulioko kwenye lango la bahari, ufanyao biashara na mataifa mengi ya pwani, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: 
“ ‘Ee Tiro, wewe umesema, 
“Mimi ni mkamilifu katika uzuri.” 
 4 Mipaka yako ilikuwa katika moyo wa bahari, 
wajenzi wako walikamilisha uzuri wako. 
 5 Walizifanya mbao zako zote 
kwa misunobari itokayo Seniri;* Yaani Hermoni. 
walichukua mierezi kutoka Lebanoni 
kukutengenezea mlingoti. 
 6 Walichukua mialoni toka Bashani 
wakakutengenezea makasia yako; 
kwa miti ya msanduku 
kutoka pwani ya Kitimu 
wakatengeneza sitaha† Yaani sakafu ya merikebu au mashua.  yako 
na kuipamba kwa pembe za ndovu. 
 7 Kitani safi kilichotariziwa kutoka Misri kilikuwa tanga lako, 
nacho kilikuwa bendera yako; 
chandarua chako kilikuwa cha rangi ya buluu na ya zambarau 
kutoka visiwa vya Elisha. 
 8 Watu kutoka Sidoni na Arvadi walikuwa wapiga makasia yako; 
watu wako wenye ustadi, ee Tiro, 
walikuwa ndio mabaharia wako. 
 9 Wazee wa Gebali‡ Yaani Bubilo, mji wa zamani sana wa Ufoinike (kama kilomita 80 kaskazini mwa Beiruti). pamoja na mafundi stadi 
walikuwa mafundi wako melini. 
Meli zote za baharini na mabaharia wao 
walikuja kwako ili kubadilishana bidhaa zako. 
 10 “ ‘Watu wa Uajemi, Ludi na Putu 
walikuwa askari katika jeshi lako. 
Walitundika ngao zao na chapeo zao kwenye kuta zako, 
wakileta fahari yako. 
 11 Watu wa Arvadi na wa Heleki 
walikuwa juu ya kuta zako pande zote; 
watu wa Gamadi 
walikuwa kwenye minara yako. 
Walitundika ngao zao kuzizunguka kuta zako; 
wakaukamilisha uzuri wako. 
 12 “ ‘Tarshishi walifanya biashara nawe kwa sababu ya utajiri wako mkubwa wa bidhaa, walibadilisha fedha, chuma, bati na risasi kwa mali zako. 
 13 “ ‘Uyunani, Tubali na Mesheki, walifanya biashara nawe, walibadilisha watumwa na vyombo vya shaba kwa bidhaa zako. 
 14 “ ‘Watu wa Beth-Togarma walibadilisha farasi wa mizigo, farasi wa vita na nyumbu kwa mali zako. 
 15 “ ‘Watu wa Dedani§ Yaani Rhodes. walifanya biashara nawe, watu wengi wa nchi za pwani walikuwa wachuuzi wako, walikulipa kwa pembe za ndovu na mpingo. 
 16 “ ‘Watu wa Aramu walifanya biashara nawe kwa ajili ya wingi wa kazi za mikono yako, wakibadilishana kwa almasi, vitambaa vya rangi ya zambarau, vitambaa vilivyotariziwa, kitani safi, matumbawe* Yaani marijani, jiwe laini la pwani au baharini, kama mawe ya chokaa. na akiki nyekundu. 
 17 “ ‘Yuda na Israeli walifanya biashara nawe, walibadilishana kwa ngano kutoka Minithi, mtama, asali, mafuta na zeri ya kuponyeshea. 
 18 “ ‘Dameski, kwa sababu ya wingi wa kazi za mikono yako na ukuu wa utajiri wa mali, walifanya biashara nawe wakibadilishana mvinyo kutoka Helboni na sufu kutoka Zahari. 
 19 “ ‘Wadani na Wayunani kutoka Uzali, walikuletea mali za biashara, nao wakabadilishana nawe chuma kilichofuliwa, mdalasini na mchaichai. 
 20 “ ‘Dedani alifanya biashara nawe kwa matandiko ya farasi. 
 21 “ ‘Arabuni na wakuu wote wa Kedari walikuwa wanunuzi wako waliobadilishana bidhaa zako na wana-kondoo, kondoo dume na mbuzi. 
 22 “ ‘Wafanyabiashara wa Sheba na wa Raama walifanya biashara nawe, wakabadilishana bidhaa zako na aina zote za vikolezi, vito vya thamani na dhahabu. 
 23 “ ‘Harani, Kane na Edeni na wafanyabiashara wa Sheba, Ashuru na Kilmadi walifanya biashara nawe.  24 Kwenye soko lako, walifanya biashara nawe kwa mavazi mazuri, vitambaa vya buluu, nguo za kutariziwa na mazulia ya rangi mbalimbali yenye kamba zilizosokotwa na kuwekwa mafundo imara. 
 25 “ ‘Merikebu za Tarshishi ndizo 
zinazokusafirishia bidhaa zako. 
Umejazwa shehena kubwa 
katika moyo wa bahari. 
 26 Wapiga makasia wako wanakupeleka 
mpaka kwenye maji makavu. 
Lakini upepo wa mashariki umekuvunja vipande vipande 
katika moyo wa bahari. 
 27 Utajiri wako, bidhaa zako na mali zako, 
mabaharia wako, manahodha wako, 
mafundi wako wa meli, 
wafanyabiashara wako na askari wako wote, 
na kila mmoja aliyeko melini 
atazama kwenye moyo wa bahari 
siku ile ya kuvunjika kwa meli yako. 
 28 Nchi za pwani zitatetemeka 
wakati mabaharia wako watakapopiga kelele. 
 29 Wote wapigao makasia 
wataacha meli zao, 
mabaharia wote na wanamaji wote 
watasimama pwani. 
 30 Watapaza sauti zao 
na kulia sana kwa ajili yako; 
watajitupia mavumbi juu ya vichwa vyao 
na kujivingirisha kwenye majivu. 
 31 Watanyoa nywele zao kwa ajili yako, 
nao watavaa nguo za magunia. 
Watakulilia kwa uchungu wa moyo 
na kwa maombolezo makuu. 
 32 Watakapokuwa wanalia na kuomboleza juu yako, 
watafanya maombolezo kukuhusu wakisema: 
“Ni nani aliyepata kuangamizwa kama Tiro, 
katika moyo wa bahari?” 
 33 Wakati bidhaa zako zilipotoka baharini, 
ulitosheleza mataifa mengi; 
kwa wingi wa utajiri wako na bidhaa zako 
ulitajirisha wafalme wa dunia. 
 34 Sasa umevunjavunjwa na bahari, 
katika vilindi vya maji, 
bidhaa zako na kundi lako lote 
vimezama pamoja nawe. 
 35 Wote waishio katika nchi za pwani 
wanakustaajabia; 
wafalme wao wanatetemeka kwa hofu kuu, 
nazo nyuso zao zimekunjamana kwa woga. 
 36 Wafanyabiashara miongoni mwa mataifa wanakucheka; 
umefikia mwisho wa kutisha 
nawe hutakuwepo tena.’ ”