28
Maandalizi Ya Daudi Ya Kujenga Hekalu
1 Daudi akawaita maafisa wote wa Israeli wakusanyike huko Yerusalemu: yaani, maafisa walio juu ya makabila, majemadari wa vikosi katika utumishi wa mfalme, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, maafisa wanaosimamia mali zote na mifugo ya mfalme na wanawe, wakiwemo maafisa wa jumba la kifalme, mashujaa na askari wote walio hodari.
2 Mfalme Daudi akainuka na kusema: “Nisikilizeni ndugu zangu nanyi watu wangu. Nilikuwa na nia ya kujenga nyumba ili iwe mahali pa kukaa Sanduku la Agano la Bwana kwa ajili ya kuwa mahali pa kuwekea miguu ya Mungu wetu, nami nikafanya maandalizi ya kuijenga. 3 Lakini Mungu akaniambia, ‘Wewe hutajenga nyumba kwa Jina langu, kwa sababu wewe umepigana vita na umemwaga damu.’
4 “Hata hivyo, Bwana, Mungu wa Israeli, alinichagua mimi kutoka jamaa yangu yote niwe mfalme juu ya Israeli milele. Alimchagua Yuda kuwa kiongozi na kutoka nyumba ya Yuda akaichagua jamaa yangu na kutoka wana wa baba yangu ikampendeza kunifanya niwe mfalme juu ya Israeli yote. 5 Miongoni mwa wanangu wote, naye Bwana amenipa wengi, amemchagua Solomoni mwanangu ili kukikalia kiti cha enzi cha ufalme wa Bwana juu ya Israeli. 6 Aliniambia, ‘Solomoni mwanao ndiye atakayejenga nyumba yangu na nyua zangu, kwa maana nimemchagua yeye kuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake. 7 Nitaufanya imara ufalme wake milele kama akiendelea kuzishika amri zangu na sheria zangu, kama afanyavyo hivi leo.’
8 “Hivyo basi ninawaagiza mbele za Israeli yote na kusanyiko hili la Bwana naye Mungu wetu akiwa anasikia: Kuweni na bidii kuzifuata amri za Bwana Mungu wenu, ili mpate kumiliki nchi hii nzuri na kuwaachia wana wenu kuwa urithi milele.
9 “Nawe Solomoni mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa kujitoa kwa moyo wote na kwa nia ya kumkubali, kwa maana Bwana huuchunguza kila moyo na kujua kila kusudi la kila fikira. Ukimtafuta, ataonekana kwako; bali kama ukimwacha, yeye atakukataa milele. 10 Angalia basi, kwa maana Bwana amekuchagua wewe ili ujenge Hekalu kuwa mahali patakatifu. Uwe hodari ukafanye kazi hiyo.”
11 Ndipo Daudi akampa Solomoni mwanawe kielelezo kwa ajili ya ukumbi wa Hekalu, nyumba zake, vyumba vyake vya hazina, ghorofa zake, vyumba vyake vya ndani na mahali pa kufanyia upatanisho. 12 Akampa vielelezo vya yote Roho alikuwa ameviweka moyoni mwake kwa ajili ya kumbi za Hekalu la Bwana na vyumba vyote vilivyolizunguka, kwa ajili ya hazina za Hekalu la Mungu na kwa hazina za vitu vilivyowekwa wakfu. 13 Mfalme pia akampa Solomoni maelekezo kwa ajili ya migawanyo ya huduma za makuhani na Walawi, pia kwa ajili ya kazi zote za huduma katika Hekalu la Bwana. Akampa pia maelezo kuhusu vifaa vyote vya kutumika katika huduma ya Hekalu. 14 Akamwagizia uzito wa dhahabu kwa ajili ya vitu vyote vya dhahabu vya kutumika katika huduma mbalimbali, uzito wa fedha kwa ajili ya vitu vyote vya fedha vya kutumika katika huduma mbalimbali. 15 Uzito wa dhahabu kwa ajili ya vinara vya dhahabu na taa zake, kukiwa na uzito kwa ajili ya kila kinara na taa zake, pamoja na uzito wa fedha kwa ajili ya kila kinara cha fedha na taa zake, kulingana na matumizi ya kila kinara; 16 uzito wa dhahabu kwa ajili ya meza ya mikate iliyowekwa wakfu, uzito wa fedha kwa ajili ya meza ya fedha; 17 uzito wa dhahabu safi kwa ajili ya nyuma, mabakuli ya kunyunyizia na vikombe, masinia; uzito wa dhahabu kwa ajili ya kila bakuli la dhahabu; uzito wa fedha kwa ajili ya kila bakuli la fedha; 18 na uzito wa dhahabu safi kwa ajili ya madhabahu ya kufukizia uvumba. Pia alimpa kielelezo kwa ajili ya gari, yaani, wale makerubi wa dhahabu waliokunjua mbawa zao na kuweka kivuli juu ya Sanduku la Agano la Bwana.
19 Daudi akasema, “Hii yote, ninayo kwa maandishi kutoka mkononi mwa Bwana ulio juu yangu, naye amenipa ufahamu kwa ajili ya habari zote za kielelezo hiki.”
20 Daudi pia akamwambia Solomoni mwanawe, “Uwe hodari na moyo mkuu, ukafanye kazi hii. Usiogope wala usifadhaike, kwa maana Bwana aliye Mungu, Mungu wangu yu pamoja nawe. Hatakuacha wala hatakupungukia mpaka kazi hii yote kwa ajili ya utumishi wa Hekalu la Bwana itakapokamilika. 21 Migawanyo ya makuhani na Walawi iko tayari kwa ajili ya kazi yote katika Hekalu la Mungu, naye kila mtu mwenye moyo wa kupenda mwenye ustadi katika aina yoyote ya ufundi atakusaidia katika kazi yote. Maafisa na watu wote watatii kila agizo lako.”