Waefeso
1
Salamu
1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu:
Kwa watakatifu walioko Efeso, walio waaminifu katika Kristo Yesu:
2 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.
Baraka Za Kiroho Katika Kristo Yesu
3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo. 4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo 5 alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe. 6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa. 7 Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake 8 aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote. 9 Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo, 10 ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani, kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.
11 Katika Kristo sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake, 12 ili kwamba, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Kristo, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake. 13 Ninyi pia mliingia ndani ya Kristo mliposikia Neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Mkiisha kuamini, ndani yake mlitiwa muhuri, yaani, Roho Mtakatifu mliyeahidiwa, 14 yeye ambaye ni amana yetu akituhakikishia urithi wetu hadi ukombozi wa wale walio milki ya Mungu kwa sifa ya utukufu wake.
Shukrani Na Maombi
15 Kwa sababu hii, tangu niliposikia juu ya imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watakatifu wote, 16 sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu. 17 Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi. 18 Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu 19 na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno 20 aliyoitumia katika Kristo alipomfufua kutoka kwa wafu, na akamketisha mkono wake wa kuume huko mbinguni, 21 juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia. 22 Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya Kanisa, 23 ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.