| Chapter 12 |
1 | Wakati huo, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano siku ya Sabato. Basi, wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakala punje zake. |
2 | Mafarisayo walipoona hayo, wakamwambia Yesu, "Tazama, wanafunzi wako wanafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato." |
3 | Yesu akawajibu, "Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? |
4 | Yeye aliingia katika Nyumba ya Mungu pamoja na wenzake, wakala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Yeye wala hao wenzake hawakuruhusiwa kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani peke yao. |
5 | Au je, hamjasoma katika Sheria kwamba kila siku ya Sabato makuhani huivunja Sheria Hekaluni, lakini hawafikiriwi kuwa na hatia? |
6 | Basi, nawaambieni kwamba hapa pana kikuu*fd* kuliko Hekalu. |
7 | Kama tu mngejua maana ya maneno haya: `Nataka huruma wala si dhabihu`, hamngewahukumu watu wasio na hatia. |
8 | Maana Mwana wa Mtu ni Bwana wa Sabato." |
9 | Yesu alitoka hapo, akaenda katika sunagogi lao. |
10 | Kulikuwa na mtu mmoja mwenye mkono uliopooza. Basi, watu wakamwuliza Yesu, "Je, ni halali kumponya mtu siku ya Sabato?" Walimwuliza hivyo wapate kisa cha kumshtaki. |
11 | Lakini Yesu akawaambia, "Tuseme mmoja wenu ana kondoo wake ambaye ametumbukia shimoni; je, hatamshika na kumtoa humo siku ya Sabato? |
12 | Mtu ana thamani kuliko kondoo! Basi, ni halali kutenda mema siku ya Sabato." |
13 | Kisha akamwambia yule mtu, "Nyosha mkono wako." Akaunyosha, nao ukawa mzima kabisa kama ule mwingine. |
14 | Basi, Mafarisayo wakatoka nje, wakashauriana jinsi watakavyomwangamiza Yesu. |
15 | Lakini Yesu alipojua jambo hilo, akatoka mahali pale. Watu wengi walimfuata, akawaponya wagonjwa wote, |
16 | akawaamuru wasiwaambie watu habari zake, |
17 | ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: |
18 | "Hapa ni mtumishi wangu niliyemteua, mpendwa wangu anipendezaye moyoni. Nitaiweka Roho yangu juu yake, naye atatangaza hukumu yangu kwa mataifa yote. |
19 | Hatakuwa na ubishi wala kupiga kelele, wala sauti yake haitasikika barabarani. |
20 | Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi ufukao moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya hukumu ya haki itawale. |
21 | Katika jina lake mataifa yatakuwa na tumaini." |
22 | Hapo watu wakamletea Yesu kipofu mmoja ambaye alikuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo. Yesu akamponya hata, akaweza kusema na kuona. |
23 | Umati wote wa watu ulishangaa ukasema, "Je, huenda ikawa huyu ndiye Mwana wa Daudi?" |
24 | Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, wakasema, "Mtu huyu anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo." |
25 | Yesu, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, "Ufalme wowote uliogawanyika makundimakundi yanayopingana, hauwezi kudumu, na mji wowote au jamaa yoyote iliyogawanyika makundimakundi yanayopingana, itaanguka. |
26 | Ikiwa Shetani anamfukuza Shetani, anajipinga mwenyewe. Basi, ufalme wake utasimamaje? |
27 | Ninyi mnasema ati nawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli; je, watoto wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo wao ndio watakaowahukumu ninyi. |
28 | Lakini ikiwa ninawafukuza pepo kwa nguvu ya Roho wa Mungu, basi jueni kwamba Ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu. |
29 | "Au, anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang`anya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyang`anya mali yake. |
30 | "Yeyote asiyejiunga nami, anapingana nami; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya. |
31 | Kwa sababu hiyo, nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu. |
32 | Tena, asemaye neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa, lakini yule asemaye neno la kumpinga Roho Mtakatifu, hatasamehewa, wala katika ulimwengu huu, wala katika ulimwengu ujao. |
33 | "Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake yatakuwa mema; ufanyeni kuwa mbaya na matunda yake yatakuwa mabaya. Mti hujulikana kwa matunda yake. |
34 | Enyi kizazi cha nyoka! Mnawezaje kusema mambo mema hali ninyi ni waovu? Maana mtu husema kutokana na yale yaliyojaa moyoni. |
35 | Mtu mwema hutoa mambo mema katika hazina yake njema; na mtu mbaya hutoa mambo mabaya katika hazina yake mbaya. |
36 | "Basi, nawaambieni, Siku ya hukumu watu watapaswa kujibu juu ya kila neno lisilofaa wanalosema. |
37 | Maana kwa maneno yako, utakubaliwa kuwa mwadilifu, na kwa maneno yako, utahukumiwa kuwa na hatia." |
38 | Kisha baadhi ya walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamwambia Yesu, "Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako." |
39 | Naye akawajibu, "Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara; hamtapewa ishara nyingine, ila tu ile ishara ya nabii Yona. |
40 | Jinsi Yona alivyokaa siku tatu kutwa kucha tumboni mwa nyangumi, ndivyo naye Mwana wa Mtu atakavyokaa ndani ya ardhi siku tatu kutwa kucha. |
41 | Watu wa Ninewi watatokea siku ya hukumu, nao watakihukumu kizazi hiki kwamba kina hatia. Maana Waninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona, na kumbe hapa kuna kikuu kuliko Yona! |
42 | Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atakihukumu kwamba kina hatia. Maana yeye alisafiri kutoka mbali akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni, na kumbe hapa kuna kikuu*fe* kuliko Solomoni. |
43 | "Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani akitafuta mahali pa kupumzika asipate. |
44 | Hapo hujisemea: `Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka.` Lakini anaporudi na kuikuta tupu, imefagiwa na kupambwa, |
45 | huenda kuwachukua pepo wengine saba, wabaya kuliko yeye; na wote huja wakamwingia huyo mtu. Na hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya kuliko hapo mwanzo. Ndivyo itakavyokuwa kwa watu hawa waovu." |
46 | Yesu alikuwa bado anasema na umati wa watu wakati mama yake na ndugu zake walipofika na kusimama nje, wakitaka kusema naye. |
47 | Basi, mtu mmoja akamwambia, "Mama yako na ndugu zako wako nje, wanataka kusema nawe." |
48 | Lakini Yesu akamjibu mtu huyo, "Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni kina nani?" |
49 | Kisha akaunyosha mkono wake kuelekea wanafunzi wake, akasema, "Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu! |
50 | Maana yeyote anayefanya anavyotaka Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu, dada yangu na mama yangu." |