| Chapter 1 |
1 | Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu. |
2 | Waliandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo. |
3 | Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango, |
4 | ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa. |
5 | Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha Abia. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni. |
6 | Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama. |
7 | Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana. |
8 | Siku moja, ilipokuwa zamu yake ya kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu, |
9 | Zakariya alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani. |
10 | Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani. |
11 | Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani. |
12 | Zakariya alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. |
13 | Lakini malaika akamwambia, "Zakariya, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane. |
14 | Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. |
15 | Atakuwa mkuu mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake. |
16 | Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao. |
17 | Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake." |
18 | Zakariya akamwambia huyo malaika, "Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu." |
19 | Malaika akamjibu, "Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu, na nimetumwa niseme nawe, nikuletee hii habari njema. |
20 | Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia." |
21 | Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakariya huku wakishangaa juu ya kukawia kwake Hekaluni. |
22 | Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono Hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu. |
23 | Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani. |
24 | Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema: |
25 | "Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu." |
26 | Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, |
27 | kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. |
28 | Malaika akamwendea, akamwambia, "Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe." |
29 | Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini? |
30 | Malaika akamwambia, "Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. |
31 | Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu. |
32 | Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. |
33 | Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho." |
34 | Maria akamjibu, "Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?" |
35 | Malaika akamjibu, "Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. |
36 | Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa. |
37 | Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu." |
38 | Maria akasema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema." Kisha yule malaika akaenda zake. |
39 | Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yuda. |
40 | Huko, aliingia katika nyumba ya Zakariya, akamsalimu Elisabeti. |
41 | Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifiu, |
42 | akasema kwa sauti kubwa, "Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa. |
43 | Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? |
44 | Nakwambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha. |
45 | Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokwambia." |
46 | Naye Maria akasema, |
47 | "Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu. |
48 | Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri. |
49 | Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, jina lake ni takatifu. |
50 | Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi. |
51 | Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao; |
52 | amewashusha wenye nguvu kutoka vitu vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu. |
53 | Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu. |
54 | Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake. |
55 | Kama alivyowaahidia wazee wetu Abrahamu na wazawa wake hata milele." |
56 | Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake. |
57 | Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume. |
58 | Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye. |
59 | Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakariya. |
60 | Lakini mama yake akasema, "La, sivyo, bali ataitwa Yohane." |
61 | Wakamwambia, "Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?" |
62 | Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani. |
63 | Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: "Yohane ndilo jina lake." Wote wakastaajabu. |
64 | Papo hapo midomo na ulimi wake Zakariya vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. |
65 | Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea. |
66 | Wote waliosikia mambo hayo waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: "Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?" Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye. |
67 | Zakariya, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka ujumbe wa Mungu: |
68 | "Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amekuja kuwasaidia na kuwakomboa watu wake. |
69 | Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake. |
70 | Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu, |
71 | kwamba atatuokoa mikononi mwa adui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia. |
72 | Alisema atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu. |
73 | Kiapo alichomwapia Abrahamu baba yetu, ni kwamba atatujalia sisi |
74 | tukombolewe kutoka adui zetu, tupate kumtumikia bila hofu, |
75 | kwa unyofu na uadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu. |
76 | Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake; |
77 | kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao. |
78 | Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atasababisha pambazuko angavu la ukombozi litujie kutoka juu, |
79 | na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani." |
80 | Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionyesha rasmi kwa watu wa Israeli. |