Swahili New Testament Bible

Luke 9

Luke

Return to Index

Chapter 10

1

Baada ya hayo, Bwana aliwachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawiliwawili, wamtangulie katika kila kijiji na mahali ambapo yeye mwenyewe alitaka kwenda.

2

Akawaambia, "Mavuno ni mengi, lakini wavunaji ni wachache. Kwa hivyo, mwombeni mwenye shamba atume wavunaji shambani mwake.

3

Sasa nendeni; fahamuni kwamba ninawatuma ninyi kama kondoo wanaokwenda kati ya mbwa mwitu.

4

Msichukue mfuko wa fedha, mkoba, wala viatu; msimsalimu mtu yeyote njiani.

5

Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza wasalimuni hivi: `Amani iwe katika nyumba hii!`

6

Kama akiwako mwenye kupenda amani, amani yenu itakaa naye, la sivyo, itawarudieni.

7

Kaeni katika nyumba hiyo mkila na kunywa wanavyowapeni, maana mfanyakazi anastahili mshahara wake. Msiende mara nyumba hii mara nyumba ile.

8

Kama mkifika mji fulani na watu wakiwakaribisha, kuleni wanavyowapeni.

9

Ponyeni wagonjwa walioko huko, waambieni watu: `Ufalme wa Mungu umekaribia kwenu.`

10

Lakini mkiingia katika mji wowote, wasipowakaribisheni, tokeni; nanyi mpitapo katika barabara zao semeni:

11

`Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu tunawakung`utieni. Lakini, jueni kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.`

12

Hakika nawaambieni, siku ile mji huo utapata adhabu kubwa zaidi kuliko ile ya watu wa Sodoma.

13

"Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwishavaa mavazi ya gunia kitambo, na kukaa katika majivu kuonyesha kwamba wametubu.

14

Hata hivyo, Siku ya Hukumu ninyi mtapata adhabu kubwa zaidi kuliko ile ya watu wa Tiro na Sidoni.

15

Na wewe Kafarnaumu, unataka kujikweza mpaka mbinguni? La; utaporomoshwa mpaka Kuzimu."

16

Halafu akasema, "Anayewasikiliza ninyi, ananisikiliza mimi; na anayekataa kuwapokea ninyi, anakataa kunipokea mimi. Yeyote anayekataa kunipokea, anakataa kumpokea yule aliyenituma."

17

Baadaye, wale sabini na wawili walirudi wamejaa furaha, wakisema, "Bwana, hata pepo wametutii tulipolitaja jina lako."

18

Yeye akawaambia, "Nilimwona Shetani jinsi alivyokuwa anaporomoka kama umeme kutoka mbinguni.

19

Naam, nimewapeni uwezo wa kukanyaga nyoka na ng`e, na uwezo juu ya nguvu zote za yule adui; hakuna chochote kitakachowadhuru.

20

Hata hivyo, msifurahi kwa sababu pepo wamewatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni." ic

21

Saa ileile, Yesu akafurahi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akasema, "Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, kwa kuwa umewaficha wenye hekima na elimu mambo haya, ukawafumbulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza."

22

Kisha akasema, "Baba yangu ameweka yote mikononi mwangu. Hakuna amjuaye Mwana ni nani ila Baba, wala amjuaye Baba ni nani ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana anataka kumfunulia hayo."

23

Halafu akawaelekea wafuasi wake akawaambia, "Heri wanaoona yale mnayoyaona ninyi!

24

Hakika, manabii na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona ninyi wasiyaone, na kusikia yale mnayoyasikia wasiyasikie."

25

Baadaye mwalimu mmoja wa Sheria alisimama akamwuliza akitaka kumtega, "Mwalimu, nifanye nini ili nipate uzima wa milele?"

26

Yesu akamwuliza, "Imeandikwa nini katika Sheria? Unaelewaje?"

27

Akamjibu, "Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe."

28

Yesu akawaambia, "Vema! Fanya hivyo, nawe utaishi."

29

Lakini yeye akitaka kujihakikishia kuwa mwema akamwuliza Yesu, "Na jirani yangu ni nani?"

30

Yesu akamjibu, "Mtu mmoja alikuwa anashuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Alipokuwa njiani, alivamiwa na majambazi, wakamnyang`anya mali yake na kumpiga, wakamwacha amelala pale nusu mfu.

31

Kumbe, kuhani mmoja akawa anapita barabara ileile, akamwona, akapita kando.

32

Hali kadhalika na Mlawi mmoja, alipofika mahali akamwona, akapita kando.

33

Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa anasafiri, alifika pale yule mtu alipokuwa, naye alipomwona, alimwonea huruma.

34

Akamwendea, akamtibu majeraha yake kwa kumtia mafuta na divai; na kuyafunga halafu akampandisha juu ya punda wake akampeleka katika nyumba moja ya wageni akamuuguza.

35

Kesho yake akatoa fedha dinari mbili akampa yule mwenye nyumba, akamwambia, `Muuguze mtu huyu; na chochote utakachotumia zaidi, nitakulipa nitakaporudi."`

36

Kisha Yesu akauliza, "Kati ya hao watatu, ni yupi aliyeonyesha kuwa jirani yake yule aliyevamiwa na majambazi?"

37

Yule mwalimu wa Sheria akamjibu, "Ni yule aliyemwonea huruma." Yesu akamwambia, "Nenda ukafanye vivyo hivyo."

38

Walipokuwa safarini, waliingia katika kijiji kimoja na mwanamke mmoja, aitwaye Martha, alimkaribisha nyumbani kwake.

39

Martha alikuwa na dada yake aitwaye Maria; huyu aliketi karibu na Yesu akisikiliza mafundisho yake.

40

Lakini Martha alikuwa anashughulika na mambo mengi. Basi, akamwendea Yesu, akamwambia, "Bwana, hivi hujali kwamba dada yangu ameniacha nishughulike peke yangu? Mwambie basi, anisaidie."

41

Lakini Bwana akamjibu, "Martha, Martha, unahangaika na kusumbuka kwa mambo mengi.

42

Kitu kimoja tu ni muhimu. Maria amechagua kitu bora zaidi ambacho hakuna mtu atakayemnyag`anya."

Luke 11

 

 

 

Public Domain Software by johnhurt.com