| Chapter 22 |
1 | Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa inakaribia. |
2 | Makuhani wakuu na walimu wa Sheria wakawa wanatafuta njia ya kumwua Yesu, lakini waliwaogopa watu. |
3 | Basi, Shetani akamwingia Yuda aitwae Iskarioti, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. |
4 | Yuda akaenda akajadiliana na makuhani wakuu na walinzi wa Hekalu kuhusu atakavyomsaliti Yesu kwao. |
5 | Nao wakafurahi na kupatana naye kumlipa fedha. |
6 | Yuda akakubali, na akawa anatafuta nafasi nzuri ya kumkabidhi kwao bila umati wa watu kujua. |
7 | Basi, siku ya Mikate Isiyotiwa chachu ikafika. Hiyo ndiyo siku ambayo mwana kondoo wa Pasaka huchinjwa. |
8 | Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohane, akawaambia, "Nendeni mkatuandalie karamu ili tupate kula Pasaka." |
9 | Nao wakamwuliza, "Unataka tuiandae wapi?" |
10 | Akawaambia, "Sikilizeni! Mtakapokuwa mnakwenda mjini, mtakutana na mwanamume anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka ndani ya nyumba atakayoingia. |
11 | Mwambieni mwenye nyumba: `Mwalimu anakuuliza, kiko wapi kile chumba ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?` |
12 | Naye atawaonyesheni chumba kikubwa ghorofani ambacho kimepambwa. Andalieni humo." |
13 | Basi, wakaenda, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia; wakaandaa karamu ya Pasaka. |
14 | Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula chakula pamoja na mitume wake. |
15 | Akawaambia, "Nimetamani sana kula Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. |
16 | Maana nawaambieni, sitaila tena hadi hapo itakapokamilika katika Ufalme wa Mungu." |
17 | Kisha akatwaa kikombe, akashukuru akasema, "Pokeeni, mgawanye ninyi kwa ninyi. |
18 | Kwa maana nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka Ufalme wa Mungu utakapokuja." |
19 | Halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, "Huu ni mwili wangu, unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka." |
20 | Akafanya vivyo hivyo na kikombe, baada ya chakula, akisema, "Kikombe hiki ni agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu inayomwagika kwa ajili yenu.*fd* |
21 | "Lakini, tazameni! Yule atakayenisaliti yuko nami hapa mezani. |
22 | Kweli Mwana wa Mtu anakwenda kuuawa kama ilivyopangwa, lakini ole wake mtu anayemsaliti." |
23 | Hapo wakaanza kuulizana wao kwa wao ni nani kati yao atakayefanya jambo hilo. |
24 | Kulitokea ubishi kati ya hao mitume kuhusu nani miongoni mwao anayefikiriwa kuwa mkuu zaidi kuliko wengine. |
25 | Yesu akawaambia, "Wafalme wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, nao huitwa wafadhili wa watu. |
26 | Lakini isiwe hivyo kati yenu; bali, yule aliye mkuu kati yenu ni lazima awe mdogo wa wote, na aliye kiongozi lazima awe kama mtumishi. |
27 | Kwa maana, ni nani aliye mkuu: yule anayeketi mezani kula chakula, ama yule anayetumikia? Bila shaka ni yule anayeketi mezani kula chakula! Hata hivyo, mimi niko hapa kati yenu kama mtumishi. |
28 | "Ninyi ndio mliobaki nami wakati wote wa majaribu yangu; |
29 | na, kama vile Baba yangu alivyonikabidhi Ufalme, vivyo hivyo nami nitawakabidhi ninyi Ufalme. |
30 | Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu, na mtaketi katika viti vya enzi kuyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. |
31 | "Simoni, Simoni! Sikiliza! Shetani alitaka kuwapepeta ninyi kama mtu anavyopepeta ngano. |
32 | Lakini mimi nimekuombea ili imani yako isipungue. Nawe utakaponirudia, watie moyo ndugu zako." |
33 | Naye Petro akamjibu, "Bwana, mimi niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani, na hata kufa." |
34 | Yesu akamjibu, "Nakwambia wewe Petro, kabla jogoo hajawika leo utakuwa umenikana mara tatu." |
35 | Kisha, Yesu akawauliza wanafunzi wake, "Wakati nilipowatuma bila mfuko wa fedha wala mkoba wala viatu, mlitindikiwa chochote?" Wakajibu, "La." |
36 | Naye akawaambia, "Lakini sasa, yule aliye na mfuko wa fedha auchukue; na aliye na mkoba, hali kadhalika. Na yeyote asiye na upanga, auze koti lake anunue mmoja. |
37 | Maana nawaambieni, haya maneno ya Maandiko Matakatifu: `Aliwekwa kundi moja na wahalifu,` ni lazima yatimie. Naam, yale yanayonihusu yanafikia ukamilifu wake." |
38 | Nao wakasema, "Bwana, tazama; hapa kuna panga mbili." Naye akasema, "Basi!" |
39 | Yesu akatoka, na kama ilivyokuwa desturi yake, akaenda katika mlima wa Mizeituni; wanafunzi wake wakamfuata. |
40 | Alipofika huko akawaambia, "Salini, msije mkaingia katika kishawishi." |
41 | Kisha akawaacha, akaenda umbali wa mtu kuweza kutupa jiwe, akapiga magoti, akasali: |
42 | "Baba, kama wapenda, ukiondoe kwangu kikombe hiki; hata hivyo, mapenzi yako yatimizwe, wala siyo yangu." |
43 | Hapo, malaika kutoka mbinguni, akamtokea ili kumtia moyo. |
44 | Akiwa katika uchungu mkubwa, alisali kwa bidii zaidi; na jasho likamtoka, kama matone ya damu, likatiririka mpaka chini.*fe* ic |
45 | Baada ya kusali, aliwarudia wanafunzi wake, akawakuta wamelala, kwani walikuwa na huzuni. |
46 | Akawaambia, "Mbona mnalala? Amkeni msali, msije mkaingia katika kishawishi." |
47 | Alipokuwa bado anaongea, kundi la watu likaja likiongozwa na yule aliyeitwa Yuda, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda kumsalimu Yesu kwa kumbusu. |
48 | Lakini Yesu akamwambia, "Yuda! Je, unamsaliti Mwana wa Mtu kwa kumbusu?" |
49 | Wale wanafunzi wake walipoona hayo wakasema, "Bwana, tutumie panga zetu?" |
50 | Na mmoja wao akampiga upanga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio lake la kulia. |
51 | Hapo, Yesu akasema, "Acha! Hii inatosha." Akaligusa sikio la mtu huyo akaliponya. |
52 | Kisha Yesu akawaambia makuhani wakuu, wakubwa wa walinzi wa Hekalu na wazee waliokuja kumkamata: "Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang`anyi? |
53 | Nilipokuwa pamoja nanyi kila siku Hekaluni hamkunitia nguvuni. Lakini, huu ndio wakati wenu hasa, ndio wakati wa utawala wa giza." |
54 | Basi, wakamkamata, wakamchukua na kwenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Petro akawa anamfuata nyuma kwa mbali. |
55 | Moto ulikuwa umewashwa katikati ya ua, nao wakawa wameketi pamoja Petro akiwa miongoni mwao. |
56 | Mjakazi mmoja alipomwona Petro ameketi karibu na moto, akamkodolea macho, akasema, "Mtu huyu alikuwa pia pamoja na Yesu." |
57 | Lakini Petro akakana akisema, "Wee! simjui mimi." |
58 | Baadaye kidogo, mtu mwingine akamwona Petro, akasema, "Wewe ni mmoja wao." Lakini Petro akajibu "Bwana we; si mimi!" |
59 | Kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasisitiza, "Hakika huyu alikuwa pamoja naye; ametoka Galilaya ati." |
60 | Lakini Petro akasema, "Bwana wee; sijui hata unachosema!" Na papo hapo, akiwa bado anaongea, jogoo akawika. |
61 | Bwana akageuka na kumtazama Petro, naye Petro akakumbuka yale aliyokuwa ameambiwa na Bwana: "Leo kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu." |
62 | Hapo akatoka nje, akalia sana. |
63 | Wale watu waliokuwa wanamchunga Yesu, walimpiga na kumdhihaki. |
64 | Walimfunga kitambaa usoni, wakawa wanamwuliza, "Ni nani aliyekupiga? Hebu bashiri tuone!" |
65 | Wakamtolea maneno mengi ya matusi. |
66 | Kulipokucha, kikao cha wazee wa watu kilifanyika, ambacho kilihudhuriwa na makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Yesu akaletwa mbele ya Baraza hilo. |
67 | Nao wakamwambia, "Twambie! Je, wewe ndiwe Kristo?" Lakini Yesu akawaambia, "Hata kama nikiwaambieni, hamtasadiki; |
68 | na hata kama nikiwaulizeni swali, hamtanijibu. |
69 | Lakini tangu sasa, Mwana wa Mtu atakuwa ameketi upande wa kulia wa Mungu Mwenyezi." |
70 | Hapo wote wakasema, "Ndiyo kusema wewe ni Mwana wa Mungu?" Naye akasema, "Ninyi mnasema kwamba mimi ndiye." |
71 | Nao wakasema, "Je, tunahitaji ushahidi mwingine? Sisi wenyewe tumesikia akisema kwa mdomo wake mwenyewe."sw4323 |