Swahili New Testament Bible

Romans 7

Romans

Return to Index

Chapter 8

1

Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo.

2

Maana, sheria ya Roho iletayo uzima kwa kuungana na Kristo Yesu imenikomboa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo.

3

Mungu ametekeleza jambo lile ambalo Sheria haikuweza kutekeleza kwa sababu ya udhaifu w binadamu. Mungu alimtuma Mwanae akiwa mwenye mwili sawa na miili yetu sisi wenye dhambi, ili aikabili dhambi, na kwa mwili huo akaiangamiza dhambi.

4

Mungu alifanya hivyo kusudi matakwa ya haki ya Sheria yatekelezwe kikamilifu ndani yetu sisi ambao tunaishi, si kwa nguvu za kibinadamu, bali kwa nguvu ya Roho.

5

Maana, wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya mwili, hutawaliwa na fikira za mwili. Lakini wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya Roho Mtakatifu, hutawaliwa na fikira za Roho.

6

Fikira za mwili huleta kifo; fikira za Roho huleta uzima na amani.

7

Maana, mwenye kutawaliwa na fikira za mwili ni adui wa Mungu; haitii sheria ya Mungu, wala hawezi kuitii.

8

Watu wanaotii matakwa ya mwili hawawezi kumpendeza Mungu.

9

Lakini ninyi hamuishi kufuatana na matakwa ya mwili, bali kufuatana na matakwa ya Roho, ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. Yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wake Kristo.

10

Lakini kama Kristo yumo ndani yenu, ingawa miili yenu itakufa kwa sababu ya dhambi, kwenu Roho ndiye uhai kwa sababu mmekubaliwa kuwa waadilifu.

11

Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Kristo kutoka wafu anaishi ndani yenu, basi huyo aliyemfufua Kristo kutoka wafu ataipa uzima miili yenu yenye hali ya kufa; atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.

12

Hivyo basi, ndugu zangu, tunalo jukumu, lakini si la kuishi kufuatana na maumbile ya kibinadamu.

13

Kwa maana, kama mkiishi kufuatana na matakwa ya maumbile ya kibinadamu, hakika mtakufa. Lakini, kama kwa njia ya Roho mnayaua matendo yenu maovu, basi, mtaishi.

14

Wote wanaoongozwa na Roho wa MUngu ni watoto wa Mungu.

15

Kwa maana, Roho mliyempokea si Roho mwenye kuwafanya ninyi watumwa na kuwatia tena hofu; sivyo, bali mmempokea Roho mwenye kuwafanya ninyi watoto wa Mungu, na kwa nguvu ya huyo Roho, sisi tunaweza kumwita Mungu, "Aba," yaani "Baba!"

16

Naye Roho mwenyewe anajiunga na roho zetu na kuthibitisha kwamba sisi ni watoto wa Mungu.

17

Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake.

18

Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyafananisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu.

19

Viumbe vyote vinatazamia kwa hamu Mungu awadhihirishe watoto wake.

20

Kwa maana, viumbe viliwekwa katika hali ya kutojiweza kabisa, si kwa hiari yao, ila vilifanywa hivyo kwa mapenzi ya Mungu. Hata hivyo yapo matumaini,

21

maana hivyo viumbe navyo vitaokolewa kutoka katika utumwa wa uharibifu, vishiriki uhuru mtukufu wa watoto wa Mungu.

22

Kwa maana tunajua kwamba mpaka hivi sasa, viumbe vyote vinalia kwa maumivu kama ya kujifungua mtoto.

23

Wala si hivyo viumbe peke yake, bali hata sisi tulio na huyo Roho, aliye wa kwanza wa zawadi za Mungu; sisi pia tunalalamika ndani yetu, tukitazamia kufanywa watoto wa Mungu, nazo nafsi zenu zikombolewe.

24

Maana kwa matumaini hayo sisi tumekombolewa; lakini tumaini halina maana ikiwa tunakiona kile tunachotumainia. Maana ni nani anayetumaini kile ambacho tayari anakiona?

25

Kama tunakitumaini kile ambacho hatujakiona bado, basi, tunakingojea kwa uvumilivu.

26

Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka.

27

Naye Mungu aonaye mpaka ndani ya mioyo ya watu, anajua fikira ya huyo Roho; kwani huyo Roho huwaombea watu wa Mungu kufuatana na mapenzi ya Mungu.

28

Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kufuatana na kusudi lake.

29

Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.

30

Basi, Mungu aliwaita wale aliokuwa amewateua; na hao aliowaita aliwakubali kuwa waadilifu; na hao aliowakubali kuwa waadilifu aliwashirikisha pia utukufu wake.

31

Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga?

32

Mungu hakumhurumia hata mwanae wa pekee, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote. Ikiwa amefanya hivyo, je, hatatujalia pia mema yote?

33

Ni nani atakayewashtaki wateule wa Mungu? Mungu mwenyewe huwaondolea hatia!

34

Ni nani atakayewahukumu? Hakuna! Maana Kristo ndiye aliyekufa, tena alifufuka kutoka wafu na anakaa upande wa kulia wa Mungu. Yeye anatuombea!

35

Ni nani awezaye kututenga na mapendo ya Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kuuawa?

36

Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Kwa ajili yako, twakikabili kifo kutwa kucha: tunatendewa kama kondoo wa kuchinjwa."

37

Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda.

38

Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: wala kifo, wala uhai; wala malaika, au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka;

39

Wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu kwetu kwa njia ya Kristo Yesu Bwana wetu.

Romans 9

 

 

 

Public Domain Software by johnhurt.com