| Chapter 10 |
1 | Ndugu zangu, ninataka na kutazamia kwa moyo wangu wote hao wananchi wenzangu wakombolewe. Tena nawaombea kwa Mungu daima. |
2 | Maana naweza kuthibitisha kwa niaba yao kwamba wanayo bidii ya kumtafuta Mungu; lakini bidii hiyo haikujengwa juu ya ujuzi wa kweli. |
3 | Maana hawakufahamu jinsi Mungu anavyowafanya watu wawe waadilifu, na wamejaribu kuanzisha mtindo wao wenyewe, na hivyo hawakuikubali njia hiyo ya Mungu ya kuwafanya wawe waadilifu. |
4 | Maana kwa kuja kwake Kristo, Sheria imefikia kikomo chake, ili kila mtu anayeamini akubaliwe kuwa mwadilifu. |
5 | Kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa kuitii Sheria, Mose aliandika hivi: "Mtu yeyote anayetimiza matakwa ya Sheria ataishi." |
6 | Lakini, kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa njia ya imani, yasemwa hivi: "Usiseme moyoni mwako: `Nani atapanda mpaka mbinguni?` (yaani, kumleta Kristo chini); |
7 | wala usiseme: `Nani atashuka mpaka Kuzimu` (yaani, kumleta Kristo kutoka kwa wafu)." |
8 | Maandiko Matakatifu yesema hivi, "Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako" nao ndio ile imani tunayoihubiri. |
9 | Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka wafu, utaokoka. |
10 | Maana tunaamini kwa moyo na kukubaliwa kuwa waadilifu; na tunakiri kwa midomo yetu na kuokolewa. |
11 | Maandiko Matakatifu yasema: "Kila amwaminiye hatakuwa na sababu ya kuaibika." |
12 | Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao. |
13 | Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa." |
14 | Basi, watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri? |
15 | Na watu watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Ni jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!" |
16 | Lakini wote hawakuipokea hiyo Habari Njema. Maana Isaya alisema: "Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?" |
17 | Hivyo basi, imani inatokana na kuusikiliza ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo. |
18 | Lakini nauliza: je, hawakuusikia huo ujumbe? Naam, waliusikia; kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Sauti yao imeenea duniani kote; maneno yao yamefika mpaka kingo za ulimwengu." |
19 | Tena nauliza: je, yawezekana kwamba watu wa Israeli hawakufahamu? Mose mwenyewe ni kwa kwanza kujibu: "Nitawafanyeni mwaonee wivu watu ambao si taifa; nitawafanyeni muwe na hasira juu ya taifa la watu wapumbavu." |
20 | Tena Isaya anathubutu hata kusema: "Wale ambao hawakunitafuta wamenipata; nimejionyesha kwao wasiouliza habari zangu." |
21 | Lakini kuhusu Israeli anasema: "Mchana kutwa niliwanyoshea mikono yangu watu waasi na wasiotii." |