| Chapter 5 |
1 | Ziko habari za kuaminika kwamba kuna uzinzi miongoni mwenu; tena ni uzinzi mbaya ambao haujapata kuwako hata kati ya watu wasiomjua Mungu. Nimeambiwa eti mmoja wenu anaishi na mke wa baba yake! |
2 | Mnawezaje kujivuna? Ingekuwa afadhali kwenu kuomboleza, na huyo aliyefanya kitu hicho aondolewe miongoni mwenu. |
3 | Nami, kwa upande wangu, ingawa kwa mwili niko mbali nanyi, hata hivyo kwa roho niko hapo pamoja nanyi: na hivyo, kama vile nipo hapo, nimekwisha mhukumu huyo aliyefanya jambo hilo la aibu. |
4 | Wakati mnapokusanyika pamoja kwa jina la Bwana Yesu, nami nikiwa pamoja nanyi kwa roho, basi, kwa uwezo wa Bwana wetu Yesu, |
5 | mkabidhini mtu huyo kwa Shetani ili mwili wake uharibiwe na roho yake iweze kuokolewa Siku ile ya Bwana. |
6 | Majivuno yenu hayafai! Je, hamjui kwamba chachu kidogo huchachusha donge lote la unga? |
7 | Jitakaseni, mkatupe mbali chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu kama mnavyopaswa kuwa; maana, Kristo, Pasaka yetu, amekwisha tolewa tambiko. |
8 | Basi, tufanye karamu hiyo si kwa chachu ile ya kale, chachu ya ubaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, mkate wa usafi na kweli. |
9 | Niliwaandikia katika barua yangu msishirikiane na wazinzi. |
10 | Ukweli ni kwamba sikuwa na maana ya watu wote duniani walio wazinzi, wachoyo, walaghai na wenye kuabudu sanamu. Maana, ili kuwaepa hao wote ingewalazimu ninyi kuihama dunia hii kabisa! |
11 | Nilichoandika ni hiki: msishirikiane na ndugu Mkristo aliye mzinzi, mchoyo, mwenye kuabudu sanamu, mchongezi mlevi na mlaghai. Mtu wa namna hiyo, hata kula msile naye. |
12 | Je, ni shauri langu kuwahukumu watu walio nje? Hao Mungu atawahukumu. Je, ninyi hampaswi kuwahukumu wale walio katika jamii yenu ninyi wenyewe? |
13 | Mfukuzeni mbali nanyi huyo mwovu! |