| Chapter 12 |
1 | Ndugu, kuhusu vipaji vya kiroho, napenda mfahamu vizuri mambo haya: |
2 | Mnajua kwamba, kabla ya kuongoka kwenu, mlitawaliwa na kupotoshwa na sanamu tupu. |
3 | Basi, jueni kwamba mtu yeyote anayeongozwa na Roho wa Mungu hawezi kusema: "Yesu alaaniwe!" Hali kadhalika, mtu yeyote hawezi kusema: "Yesu ni Bwana," asipoongozwa na Roho Mtakatifu. |
4 | Vipaji vya kiroho ni vya namna nyingi, lakini Roho avitoaye ni mmoja. |
5 | Kuna namna nyingi za kutumikia, lakini Bwana anayetumikiwa ni mmoja. |
6 | Kuna namna mbalimbali za kufanya kazi ya huduma, lakini Mungu ni mmoja, anayewezesha kazi zote katika wote. |
7 | Kila mtu hupewa mwangaza wa Roho kwa faida ya wote. |
8 | Roho humpa mmoja ujumbe wa hekima, na mwingine ujumbe wa elimu apendavyo Roho huyohuyo. |
9 | Roho huyohuyo humpa mmoja imani, na humpa mwingine kipaji cha kuponya; |
10 | humpa mmoja kipaji cha kufanya miujiza, mwingine kipaji cha kusema ujumbe wa Mungu, mwingine kipaji cha kubainisha vipaji vitokavyo kwa Roho na visivyo vya Roho; humpa mmoja kipaji cha kusema lugha ngeni, na mwingine kipaji cha kuzifafanua. |
11 | Hizo zote ni kazi za Roho huyohuyo mmoja, ambaye humpa kila mtu kipaji tofauti, kama apendavyo mwenyewe. |
12 | Kama vile mwili ulivyo mmoja wenye viungo vingi, na viungo hivyo vyote--ingawaje ni vingi--hufanya mwili mmoja, ndivyo ilivyo pia kwa Kristo. |
13 | Maana sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika mwili huo mmoja; na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja. |
14 | Mwili hauna kiungo kimoja tu, bali una viungo vingi. |
15 | Kama mguu ungejisemea: "Kwa kuwa mimi si mkono, basi mimi si mali ya mwili", je, ungekoma kuwa sehemu ya mwili? La hasha! |
16 | Kama sikio lingejisemea: "Kwa vile mimi si jicho, basi mimi si mali ya mwili", je, kwa hoja hiyo lingekoma kuwa sehemu ya mwili? La! |
17 | Kama mwili wote ungekuwa jicho, sikio lingekuwa wapi? Na kama mwili wote ungekuwa sikio, mtu angewezaje kunusa? |
18 | Lakini kama ilivyo, Mungu alizipanga sehemu hizo tofauti katika mwili kama alivyopenda. |
19 | Kama sehemu zote zingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? |
20 | Ukweli ni kwamba, sehemu za mwili ni nyingi, lakini mwili ni mmoja. |
21 | Basi, jicho haliwezi kuuambia mkono: "Sikuhitaji wewe", wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu: "Siwahitaji ninyi." |
22 | Zaidi ya hayo, inaonekana kwamba sehemu zile za mwili zinazoonekana kuwa ni dhaifu ndizo zilizo muhimu zaidi. |
23 | Tena, viungo vile tunavyovifikiria kuwa havistahili heshima kubwa, ndivyo tunavyovitunza kwa uangalifu zaidi; viungo vya mwili ambavyo havionekani kuwa vizuri sana, huhifadhiwa zaidi, |
24 | ambapo viungo vingine havihitaji kushughulikiwa. Mungu mwenyewe ameuweka mwili katika mpango, akakipa heshima zaidi kiungo kile kilichopungukiwa heshima, |
25 | ili kusiweko na utengano katika mwili bali viungo vyote vishughulikiane. |
26 | Kama kiungo kimoja kinaumia viungo vyote huumia pamoja nacho. Kiungo kimoja kikisifiwa viungo vingine vyote hufurahi pamoja nacho. |
27 | Basi, ninyi nyote ni mwili wa Kristo; kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo. |
28 | Mungu ameweka katika kanisa: kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu; kisha ameweka wale wenye kipaji cha kufanya miujiza, kuponya, kusaidia; viongozi na wenye kusema lugha ngeni. |
29 | Je, wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni walimu? Wote ni wenye kipaji cha kufanya miujiza? |
30 | Je, wote ni wenye kipaji cha kuponya? Wote ni wenye kipaji cha kusema lugha ngeni? Je, wote hufafanua lugha? |
31 | Muwe basi, na tamaa ya kupata vipaji muhimu zaidi. Nami sasa nitawaonyesheni njia bora zaidi kuliko hizi zote. |