| Chapter 5 |
1 | Maana tunajua kwamba hema hii ambayo ndani yake tunaishi sasa hapa duniani, yaani mwili wetu, itakapong`olewa, Mungu atatupa makao mengine mbinguni, nyumba ya milele isiyotengenezwa kwa mikono. |
2 | Na sasa, katika hali hii, tunaugua, tukitazamia kwa hamu kubwa kuvikwa makao yetu yaliyo mbinguni. |
3 | Naam, tunapaswa kuvikwa namna hiyo ili tusije tukasimama mbele ya Mungu bila vazi. |
4 | Tukiwa bado katika hema hii ya duniani, tunalia kwa kukandamizwa; si kwamba tunataka kuuvua mwili huu wa kufa, ila tuna hamu ya kuvalishwa ule usiokufa, ili kile chenye kufa kimezwe kabisa na uhai. |
5 | Mungu mwenyewe alitutayarishia mabadiliko hayo, naye ametupa Roho wake awe dhamana ya yote aliyotuwekea. |
6 | Tuko imara daima. Tunajua kwamba kuishi katika mwili huu tu ni kukaa mbali na Bwana. |
7 | Maana tunaishi kwa imani, na si kwa kuona. |
8 | Lakini tuko imara na tungependelea hata kuyahama makao haya, tukahamie kwa Bwana. |
9 | Lakini jambo la maana zaidi, tunataka kumpendeza, iwe tunaishi hapa duniani au huko. |
10 | Maana sote ni lazima tusimame mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apokee anayostahili kwa matendo aliyoyafanya wakati alipokuwa anaishi duniani, mema au mabaya. |
11 | Basi, sisi tunajua umuhimu wa kumcha Bwana, na hivyo tunajitahidi kuwavuta watu. Mungu anatujua waziwazi, nami natumaini kwamba nanyi pia mnatujua kinaganaga. |
12 | Si kwamba tunajaribu tena kujipendekeza kwenu, ila tunataka kuwapa ninyi sababu zetu za kuona fahari juu yenu, ili mpate kuwajibu wale wanaojivunia hali yao ya nje zaidi kuliko jinsi walivyo moyoni. |
13 | Ikiwa tumeonekana kuwa wendawazimu, hiyo ni kwa ajili ya Mungu; na ikiwa tunazo akili zetu timamu, hiyo ni kwa faida yenu. |
14 | Maana mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili ya wote, na hiyo ina maana kwamba wote wanashiriki kifo chake. |
15 | Alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wanaoishi wasiishi kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa kwa ajili yao. |
16 | Basi, tangu sasa, sisi hatumpimi mtu yeyote kibinadamu. Hata kama kwa wakati mmoja tulimpima Kristo kibinadamu, sasa si hivyo tena. |
17 | Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo ya kale yamepita, hali mpya imefika. |
18 | Yote ni kazi ya Mungu mwenye kutupatanisha sisi naye kwa njia ya Kristo, akatupa nasi jukumu la kuwapatanisha watu naye. |
19 | Ndiyo kusema: Mungu, amekuwa akiupatanisha ulimwengu naye kwa njia ya Kristo, bila kutia maanani dhambi zao binadamu. Yeye ametupa ujumbe kuhusu kuwapatanisha watu naye. |
20 | Basi, sisi tunamwakilisha Kristo, naye Mungu mwenyewe anatutumia sisi kuwasihi ninyi. Tunawaombeni kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu. |
21 | Kristo hakuwa na dhambi, lakini Mungu alimfanya ahusike na dhambi kwa ajili yetu, ili sisi kwa kuungana naye, tupate kuushiriki uadilifu wake Mungu. |