| Chapter 6 |
1 | Ndugu, kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, ninyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije nanyi wenyewe mkajaribiwa. |
2 | Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo. |
3 | Mtu akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe. |
4 | Lakini kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu mwingine. |
5 | Maana kila mmoja anao mzigo wake mwenyewe wa kubeba. |
6 | Mwenye kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake. |
7 | Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna. |
8 | Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uzima wa milele. |
9 | Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake. |
10 | Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu. |
11 | Tazameni jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe. |
12 | Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha ninyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: kusudi wao wenyewe wasije wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo. |
13 | Maana, hao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki Sheria; huwataka ninyi mtahiriwe wapate kujivunia alama hiyo mwilini mwenu. |
14 | Lakini mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. |
15 | Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya. |
16 | Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli--Wateule wa Mungu. |
17 | Basi, sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni zile za Yesu. |
18 | Ndugu, nawatakieni ninyi nyote neema ya Bwana wetu Kristo. Amina. |