| Chapter 4 |
1 | Roho asema waziwazi kwamba siku za baadaye watu wengine wataitupilia mbali imani; watazitii roho danganyifu na kufuata mafundisho ya pepo. |
2 | Mafundisho ya namna hiyo yanaenezwa na watu waongo wadanganyifu, ambao dhamiri zao ziko kama zimechomwa kwa chuma cha moto. |
3 | Watu hao hufundisha kwamba ni makosa kuona na pia kula vyakula fulani. Lakini Mungu aliviumba vyakula hivyo, ili wale walio waumini na ambao wanapata kuujua ukweli, wavitumie kwa shukrani. |
4 | Kila kitu alichoumba Mungu ni chema, wala hakuna kinachohitaji kukataliwa, bali vyote vipokelewe kwa sala ya shukrani, |
5 | kwa sababu neno la Mungu na sala hukifanya kitu hicho kikubalike kwa Mungu. |
6 | Kama ukiwapa ndugu wote maagizo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, ukijiendeleza kiroho kwa maneno ya imani na mafundisho ya kweli, ambayo wewe umeyafuata. |
7 | Lakini achana na hadithi zile zisizo za kidini na ambazo hazina maana. Jizoeshe kuishi maisha ya uchaji wa Mungu. |
8 | Mazoezi ya mwili yana faida yake, lakini mazoezi ya kiroho yana faida za kila namna, maana yanatuahidia uzima katika maisha ya sasa, na pia hayo yanayokuja. |
9 | Usemi huo ni wa kusadikika kabisa na unastahili kukubaliwa. |
10 | Sisi tunajitahidi na kufanya kazi kwa bidii kwani tumemwekea tumaini letu Mungu aliye hai ambaye ni Mwokozi wa watu wote, na hasa wale wanaoamini. |
11 | Wape maagizo hayo na mafundisho hayo. |
12 | Usikubali mtu yeyote akudharau kwa sababu wewe ni kijana, lakini jitahidi uwe mfano kwa wanaoamini: katika usemi wako, mwenendo wako, upendo, imani na maisha safi. |
13 | Tumia wakati wako na juhudi yako katika kusoma hadharani Maandiko Matakatifu, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. |
14 | Usiache kukitumia kile kipaji cha Kristo ndani yako ulichopewa kwa maneno ya manabii na kwa kuwekewa mikono na wazee. |
15 | Fikiri kwa makini juu ya hayo yote na kuyatekeleza kusudi maendeleo yako yaonekane na wote. |
16 | Angalia sana mambo yako mwenyewe, na mafundisho yako. Endelea kufanya hayo maana ukifanya hivyo utajiokoa mwenyewe na wale wanaokusikiliza. |