| Chapter 1 |
1 | Mimi Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo naandika. Mimi nimechaguliwa kuijenga imani ya wateule wa Mungu na kuwaongoza waufahamu ukweli wa dini yetu, |
2 | ambayo msingi wake ni tumaini la kupata uzima wa milele. Mungu ambaye hasemi uongo, alituahidia uzima huo kabla ya mwanzo wa nyakati, |
3 | na wakati ufaao ulipowadia, akaudhihirisha katika ujumbe wake. Mimi nilikabidhiwa ujumbe huo nuutangaze kufuatana na amri ya Mungu, Mwokozi wetu. |
4 | Ninakuandikia wewe Tito, mwanangu wa kweli katika imani tunayoshiriki. Nakutakia neema na amani kutoka kwa Mungu Baba, na kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wetu. |
5 | Nilikuacha Krete ili urekebishe yale mambo ambayo hayakuwa yamekamilika bado, na kuwateua wazee wa kanisa katika kila mji. Kumbuka maagizo yangu: |
6 | mzee wa kanisa anapaswa kuwa mtu asiye na hatia; aliye na mke mmoja tu, na watoto wake wanapaswa kuwa waumini, wasiojulikana kuwa wakorofi au wakaidi. |
7 | Maana kwa vile kiongozi wa kanisa ni mkurugenzi wa kazi ya Mungu, anapaswa kuwa mtu asiye na hatia. Asiwe mwenye majivuno, mwepesi wa hasira, mlevi, mkorofi au mchoyo. |
8 | Anapaswa kuwa mkarimu na anayependa mambo mema. Anapaswa kuwa mtu mtaratibu, mwadilifu, mtakatifu na mwenye nidhamu. |
9 | Ni lazima ashike kikamilifu ujumbe ule wa kuaminika kama unavyofundishwa. Ndivyo atakavyoweza kuwatia wengine moyo kwa mafundisho ya kweli na kuyafichua makosa ya wale wanaoyapinga mafundisho hayo. |
10 | Maana, wako watu wengi, hasa wale walioongoka kutoka dini ya Kiyahudi, ambao ni wakaidi, wanaowapotosha wengine kwa upumbavu wao. |
11 | Lazima kukomesha maneno yao, kwani wanavuruga jumuiya nzima kwa kufundisha mambo ambayo hawapaswi kufundisha; wanafanya hivyo kwa nia mbaya ya kupata faida ya fedha. |
12 | Hata mmoja wa manabii wao, ambaye naye pia ni Mkrete, alisema: "Wakrete, husema uongo daima; ni kama wanyama wabaya, walafi na wavivu!" |
13 | Naye alitoboa ukweli kwa sababu hiyo, unapaswa kuwakaripia vikali, ili wawe na imani kamilifu. |
14 | Wasiendelee kushikilia hadithi tupu za Kiyahudi na maagizo ya kibinadamu yanayozuka kwa watu walioukataa ukweli. |
15 | Kila kitu ni safi kwa watu walio safi; lakini hakuna chochote kilicho safi kwa wale waliochafuliwa na wasioamini, maana dhamiri na akili zao zimechafuliwa. |
16 | Watu kama hao hujidai kwamba wanamjua Mungu, lakini kwa matendo yao humkana. Ni watu wa kuchukiza mno na wakaidi, hawafai kwa jambo lolote jema. |