| Chapter 2 |
1 | Lakini wewe unapaswa kuhubiri mafundisho safi. |
2 | Waambie wazee kwamba wanapaswa kuwa na kiasi, wawe na busara na wataratibu; wanapaswa kuwa timamu katika imani yao, upendo na uvumilivu. |
3 | Hali kadhalika waambie wanawake wazee wawe na mwenendo wa uchaji wa Mungu; wasiwe wachongezi, au watumwa wa pombe. Wanapaswa kufundisha mambo mema, |
4 | ili wawazoeze kina mama vijana kuwapenda waume zao na watoto, |
5 | wawe na kiasi na safi, waangalie vizuri mambo ya nyumbani, na wawatii waume zao, ili ujumbe wa Mungu usije ukadharauliwa. |
6 | Kadhalika, wahimize vijana wawe na kiasi. |
7 | Katika mambo yote wewe mwenyewe unapaswa kuwa mfano wa matendo mema. Uwe mnyofu na uwe na uzito katika mafundisho yako. |
8 | Maneno yako yasiwe na hitilafu yoyote ili adui zako waaibike wasipopata chochote kibaya cha kusema juu yetu. |
9 | Watumwa wanapaswa kuwatii wakuu wao na kuwapendeza katika mambo yote. Wasibishane nao, |
10 | au kuiba vitu vyao. Badala yake wanapaswa kuonyesha kwamba wao ni wema na waaminifu daima, ili, kwa matendo yao yote, wayapatie sifa njema mafundisho juu ya Mungu, Mwokozi wetu. |
11 | Maana neema ya Mungu imedhihirishwa kwa ajili ya wokovu wa watu wote. |
12 | Neema hiyo yatufunza kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia; tuwe na kiasi, tuishi maisha adili na ya kumcha Mungu katika ulimwengu huu wa sasa, |
13 | tukiwa tunangojea siku ile ya heri tunayoitumainia, wakati utakapotokea utukufu wa Mungu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo. |
14 | Yeye alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na kutufanya watu safi walio wake yeye mwenyewe, watu walio na hamu ya kutenda mema. |
15 | Basi, fundisha mambo hayo na tumia mamlaka yako yote ukiwahimiza na kuwaonya wasikilizaji wako. Mtu yeyote na asikudharau. |