Swahili New Testament Bible

Hebrews 10

Hebrews

Return to Index

Chapter 11

1

Kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayotumainia; kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona.

2

Maana wazee wa kale walipata kibali cha Mungu kwa sababu ya imani yao.

3

Kwa imani sisi tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu; vitu vinavyoonekana kutoka vitu visivyoonekana.

4

Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu iliyokuwa bora zaidi kuliko ile ya Kaini. Kwa imani yake alikubaliwa na Mungu kuwa mwadilifu; Mungu mwenyewe alizikubali sadaka zake. Kwa imani yake ingawa amekufa, bado ananena.

5

Kwa imani Henoki alichukuliwa na Mungu, asipate kufa. Hakuonekana tena kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Maandiko yasema kwamba kabla ya kuchukuliwa kwake, yeye alikuwa amempendeza Mungu.

6

Basi, pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu. Kwa maana kila mtu anayemwendea Mungu ni lazima aamini kwamba Mungu yuko, na kwamba huwatuza wale wanaomtafuta.

7

Kwa imani Noa alionywa na Mungu juu ya mambo ya baadaye ambayo hakuweza kuyaona bado. Alimtii Mungu, akajenga ile safina ambamo aliokolewa yeye pamoja na jamaa yake. Kutokana na hayo ulimwengu ulihukumiwa, naye Noa akapokea uadilifu unaotokana na imani.

8

Kwa imani Abrahamu alimtii Mungu alipoitwa aende katika nchi ambayo Mungu angempa iwe yake. Ingawa hakujua alikokuwa anakwenda, Abrahamu alihama.

9

Kwa imani aliishi kama mgeni katika nchi aliyoahidiwa na Mungu. Aliishi huko katika hema kama walivyoishi Isaka na Yakobo, ambao pia walishiriki ahadi ileile.

10

Maana Abrahamu alikuwa akingojea mji wenye misingi imara, mji ambao Mungu mwenyewe ndiye fundi aliyeubuni na kuujenga.

11

Kwa imani hata Sara aliamini kwamba Mungu hutimiza ahadi zake, kwa hiyo akajaliwa kuchukua mimba ingawaje alikuwa amepita umri.

12

Kwa hiyo, kutoka katika mtu huyo mmoja, Abrahamu, ambaye alikuwa kama amekufa, walitokea watu wengi wasiohesabika kama vile nyota za mbinguni na mchanga wa pwani.

13

Watu hawa wote walikufa wakiwa na imani. Walikufa kabla ya kupokea mambo ambayo Mungu alikuwa ameahidi, lakini kwa mbali waliyaona, wakashangilia, na kukiri wazi kwamba wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani.

14

Watu wanaosema mambo kama hayo, huonyesha wazi kwamba wanaitafuta nchi yao wenyewe.

15

Kama wangalikuwa wanaifikiria nchi walikotoka zamani, wangalipata nafasi ya kurudi huko.

16

Lakini sasa wanataka nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Ndiyo maana Mungu haoni haya wakimwita yeye Mungu wao, kwa sababu yeye mwenyewe amekwisha watayarishia mji.

17

Kwa imani, Abrahamu alimtoa mwanae Isaka sadaka wakati Mungu alipomjaribu. Huyo Abrahamu ndiye aliyekuwa amepokea ahadi ya Mungu, lakini, hata hivyo, alikubali kumtoa dhabihu mwanae wa pekee,

18

ingawa Mungu alikuwa amemwambia: "Wazawa wako watatokana na Isaka."

19

Abrahamu aliamini kwamba Mungu anaweza kuwafufua wafu: na kwa namna fulani kweli Abrahamu alimpata tena mwanae kutoka wafu.

20

Kwa imani Isaka aliwabariki Yakobo na Esau, wapate baraka zitakazokuja baadaye.

21

Kwa imani Yakobo alipokuwa karibu kufa, aliwabariki kila mmoja wa wana wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiegemea ile fimbo yake.

22

Kwa imani Yosefu alipokuwa karibu kufa, alinena juu ya kutoka kwa Waisraeli katika nchi ya Misri, na pia akawaachia maagizo kuhusu mifupa yake.

23

Kwa imani wazazi wa Mose walimficha huyo mtoto kwa muda wa miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwake. Walimwona kuwa ni mtoto mzuri, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.

24

Kwa imani Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao.

25

Aliona ni afadhali kuteseka pamoja na watu wa Mungu kuliko kufurahia raha ya dhambi kwa kitambo kidogo.

26

Alitambua kwamba kuteseka kwa ajili ya Masiha kuna faida kubwa zaidi kuliko utajiri wote wa nchi ya Misri, maana alikuwa anatazamia tuzo la baadaye.

27

Kwa imani Mose alihama kutoka nchi ya Misri bila kuogopa hasira ya mfalme; na wala hakurudi nyuma, kwani alikuwa kama mtu aliyemwona yule Mungu asiyeonekana.

28

Kwa imani aliadhimisha siku ya Pasaka, akaamuru damu inyunyizwe juu ya milango, ili yule Malaika Mwangamizi asiwaue wazaliwa wa kwanza wa Israeli.

29

Kwa imani watu wa Israeli walivuka bahari ya Shamu, kana kwamba ilikuwa nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo walikufa maji.

30

Kwa imani kuta za mji wa Yeriko zilianguka watu wa Israeli walipokwisha zunguka kwa muda wa siku saba.

31

Kwa imani Rahabu aliyekuwa malaya hakuangamia pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa sababu aliwakaribisha wale wapelelezi.

32

Basi, niseme nini zaidi? Wakati hauniruhusu kueleza juu ya Gedeoni, Baraki, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii.

33

Kwa imani hawa wote walipigana vita na wafalme, wakashinda. Walitenda mambo adili, wakapokea yale aliyoahidi Mungu. Walifunga vinywa vya simba,

34

Walizima mioto mikali, waliepuka kuuawa kwa upanga. Walikuwa dhaifu lakini walipata nguvu. Walikuwa hodari katika vita wakashinda majeshi ya kigeni.

35

Na, wanawake walioamini walirudishiwa wafu wao wakiwa wamefufuliwa. Baadhi yao walikataa kufunguliwa, wakateswa mpaka kufa ili wapate kufufuliwa na kuingia katika maisha bora zaidi.

36

Wengine walidhihakiwa na kupigwa mijeledi, na wengine walifungwa minyororo na kutupwa gerezani.

37

Walipigwa mawe, walipasuliwa vipandevipande, waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi, walikuwa watu maskini, walioteswa na kudhulumiwa.

38

Ulimwengu haukustahili kuwa na watu hao. Walitangatanga jangwani na mlimani, wakaishi katika mashimo na mapango ya ardhi.

39

Watu hawa wote walionekana kuwa mashujaa kwa sababu ya imani yao. Hata hivyo, hawakupokea yale ambayo Mungu aliwaahidia,

40

maana Mungu alikuwa ameazimia mpango ulio bora zaidi kwa ajili yetu; yaani wao wangeufikia ukamilifu wakiwa pamoja nasi.

Hebrews 12

 

 

 

Public Domain Software by johnhurt.com