| Chapter 2 |
1 | Ndugu zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwabague watu kamwe. |
2 | Tuseme mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu. |
3 | Ikiwa mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: "Keti hapa mahali pazuri," na kumwambia yule maskini: "Wewe, simama huko," au "Keti hapa sakafuni miguuni pangu," |
4 | je, huo si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya? |
5 | Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea Utawala aliowaahidia wale wanaompenda. |
6 | Lakini ninyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamizeni na kuwapeleka mahakamani? |
7 | Je, si haohao wanaolitukana hilo jina lenu zuri mlilopewa? |
8 | Kama mnaitimiza ile sheria ya Utawala kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu: "Mpende binadamu mwenzako kama unavyojipenda wewe mwenyewe", mtakuwa mnafanya vema kabisa. |
9 | Lakini mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo Sheria inawahukumu ninyi kuwa mna hatia. |
10 | Anayevunja amri mojawapo ya Sheria, atakuwa na hatia ya kuivunja Sheria yote. |
11 | Maana yuleyule aliyesema: "Usizini," alisema pia "Usiue". Kwa hiyo, hata ikiwa hukuzini lakini umeua, wewe umeivunja Sheria. |
12 | Basi, semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru. |
13 | Maana, Mungu hatakuwa na huruma atakapomhukumu mtu asiyekuwa na huruma. Lakini huruma hushinda hukumu. |
14 | Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je, hiyo imani yawezaje kumwokoa? |
15 | Tuseme kaka au dada hana nguo au chakula. |
16 | Yafaa kitu gani ninyi kuwaambia hao: "Nendeni salama mkaote moto na kushiba," bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha? |
17 | Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa. |
18 | Lakini mtu anaweza kusema: "Wewe unayo imani, mimi ninayo matendo!" Haya! Nionyeshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo yangu. |
19 | Je, wewe unaamini kwamba yuko Mungu mmoja? Sawa! Lakini hata pepo huamini hilo, na hutetemeka kwa hofu. |
20 | Mpumbavu wee! Je, wataka kuonyeshwa kwamba imani bila matendo imekufa? |
21 | Je, Abrahamu baba yetu alipataje kukubalika mbele yake Mungu? Kwa matendo yake, wakati alipomtoa mwanae Isaka sadaka juu ya madhabahu. |
22 | Waona basi, kwamba imani yake iliandamana na matendo yake; imani yake ilikamilishwa kwa matendo yake. |
23 | Hivyo yakatimia yale Maandiko Matakatifu yasemayo: "Abrahamu alimwamini Mungu na kwa imani yake akakubaliwa kuwa mtu mwadilifu; na hivyo Abrahamu akaitwa rafiki wa Mungu." |
24 | Mnaona basi, kwamba mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa matendo yake na si kwa imani peke yake. |
25 | Ilikuwa vivyo hivyo kuhusu yule malaya Rahabu; yeye alikubaliwa kuwa mwadilifu kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi na kuwasaidia waende zao kwa kupitia njia nyingine. |
26 | Basi, kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa. |