| Chapter 17 |
1 | Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na bakuli akaja, akaniambia, "Njoo, mimi nitakuonyesha adhabu aliyopewa yule mzinzi mkuu, mji ule uliojengwa juu ya maji mengi. |
2 | Wafalme wa dunia wamefanya uzinzi pamoja naye; na wakazi wa dunia wamelewa divai ya uzinzi wake." |
3 | Kisha, Roho akanikumba, akaniongoza mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke ameketi juu ya mnyama mwekundu. Mnyama huyo alikuwa ameandikwa kila mahali majina ya makufuru; alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. |
4 | Mwanamke huyo alikuwa amevaa vazi la rangi ya zambarau na nyekundu; alikuwa amejipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu. Mkononi mwake alishika kikombe cha dhahabu ambacho kilikuwa kimejaa machukizo na mambo machafu yanayoonyesha uzinzi wake. |
5 | Alikuwa ameandikwa juu ya paji la uso wake jina la fumbo "Babuloni mkuu, mama wa wazinzi na wa mambo yote ya kuchukiza sana duniani." |
6 | Nikamwona huyo mwanamke amelewa damu ya watu wa Mungu, na damu ya watu waliouawa kwa sababu ya kumtangaza Yesu. Nilipomwona nilishangaa mno. |
7 | Lakini malaika akaniambia, "Kwa nini unashangaa? Mimi nitakuambia maana iliyofichika ya mwanamke huyu na mnyama huyo amchukuaye ambaye ana vichwa saba na pembe kumi. |
8 | Huyo mnyama uliyemwona alikuwa hai hapo awali, lakini sasa amekufa. Hata hivyo, karibu sana atapanda kutoka shimoni kuzimu, lakini ataangamizwa. Wanaoishi duniani watashangaa; naam, watu wote ambao majina yao hayakupata kuandikwa katika kitabu cha uzima tangu mwanzo wa ulimwengu, watashangaa kumwona huyo mnyama ambaye hapo awali, aliishi, kisha akafa na sasa anatokea tena! |
9 | "Hapa panahitaji akili na hekima! Hivyo vichwa saba ni vilima saba, na huyo mwanamke anaketi juu yake. Vichwa hivyo pia ni wafalme saba. |
10 | Kati ya hao wafalme saba, watano wamekwisha angamia, mmoja anatawala bado, na yule mwingine bado hajafika; na atakapofika atabaki kwa muda mfupi. |
11 | Huyo mnyama ambaye alikuwa anaishi hapo awali lakini sasa haishi tena ni mfalme wa nane, naye pia ni miongoni mwa hao saba, na anakwenda zake kuharibiwa. |
12 | "Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme ambao bado hawajaanza kutawala. Lakini watapewa mamlaka ya kutawala kwa muda wa saa moja pamoja na yule mnyama. |
13 | Shabaha ya hawa kumi ni moja, na watampa yule mnyama nguvu na mamlaka yao yote. |
14 | Watapigana na Mwanakondoo, lakini Mwanakondoo pamoja na wale aliowaita na kuwachagua, ambao ni waaminifu, atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme." |
15 | Malaika akaniambia pia, "Yale maji uliyoyaona pale alipokaa yule mzinzi, ni mataifa, watu wa kila rangi na lugha. |
16 | Pembe zile kumi ulizoziona na yule mnyama watamchukia huyo mzinzi. Watachukua kila kitu alicho nacho na kumwacha uchi; watakula nyama yake na kumteketeza kwa moto. |
17 | Maana Mungu ametia mioyoni mwao nia ya kutekeleza shabaha yake, yaani kwa kukubaliana wao kwa wao na kumpa huyo mnyama mamlaka yao ya kutawala, mpaka hapo neno la Mungu litakapotimia. |
18 | "Na yule mwanamke uliyemwona ndio ule mji mkuu unaowatawala wafalme wa dunia." |