| Chapter 18 |
1 | Baada ya hayo, nilimwona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa na uwezo mkuu, na dunia ikamulikwa na mng`ao wake. |
2 | Basi, akapaaza sauti kwa nguvu akisema, "Umeanguka; Babuloni mkuu umeanguka! Sasa umekuwa makao ya mashetani na pepo wachafu; umekuwa makao ya ndege wachafu na wa kuchukiza mno. |
3 | Maana mataifa yote yalileweshwa kwa divai kali ya uzinzi wake, nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye. Nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na anasa zake zisizo na kipimo." |
4 | Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema, "Watu wangu, ondokeni kwake, ili msishirikiane naye katika dhambi zake, msije mkaipata adhabu yake. |
5 | Kwa maana dhambi zake zimekuwa nyingi mno, zimelundikana mpaka mbinguni, na Mungu ameyakumbuka maovu yake. |
6 | Mtendeeni kama alivyowatendea ninyi; mlipeni mara mbili kwa yale aliyoyatenda. Jazeni kikombe chake kwa kinywaji kikali mara mbili zaidi ya kile alichowapeni. |
7 | Mpeni mateso na uchungu kadiri ya kujigamba kwake, na kuishi kwake kwa anasa. Maana anajisemea moyoni: `Ninaketi hapa; mimi ni malkia. Mimi si mjane, wala sitapatwa na uchungu!` |
8 | Kwa sababu hiyo mabaa yake yatampata kwa siku moja: ugonjwa, huzuni na njaa. Atachomwa moto, maana Bwana Mungu mwenye kumhukumu ni Mwenye Uwezo." |
9 | Wafalme wa Dunia waliofanya uzinzi naye na kuishi naye maisha ya anasa wataomboleza na kulia wakati watakapoona moshi wa mji huo unaoteketea. |
10 | Wanasimama kwa mbali kwa sababu ya kuogopa mateso yake, na kusema, "Ole! Ole kwako Babuloni, mji maarufu na wenye nguvu! Kwa muda wa saa moja tu adhabu yako imekupata." |
11 | Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumfanyia matanga, maana hakuna mtu anayenunua tena bidhaa zao; |
12 | hakuna tena wa kununua dhahabu yao, fedha, mawe ya thamani na lulu, kitani na nguo za rangi ya zambarau, hariri na nguo nyekundu; vyombo vya kila aina ya miti ya pekee, vyombo vya pembe za ndovu, vya miti ya thamani kubwa, vya shaba, chuma na marmari; |
13 | mdalasini, viungo, ubani, manemane, udi, divai, mafuta, unga na ngano, ng`ombe na kondoo, farasi na magari ya kukokotwa, watumwa wao na hata maisha ya watu. |
14 | Wafanyabiashara wanamwambia: "Faida yote uliyotazamia imetoweka, na utajiri na fahari vimekuponyoka; hutaweza kuvipata tena!" |
15 | Wafanya biashara waliotajirika kutokana na mji huo, watasimama mbali kwa sababu ya hofu ya mateso yake, watalalamika na kuomboleza, |
16 | wakisema, "Ole! Ole kwa mji huu mkuu. Ulizoea kuvalia nguo za kitani, za rangi ya zambarau na nyekundu, na kujipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu! |
17 | Kwa saa moja tu utajiri wako umetoweka!" Halafu manahodha wote na wasafiri wao, wanamaji na wote wanaofanya kazi baharini, walisimama kwa mbali, |
18 | na walipouona moshi wa moto ule uliouteketeza, wakalia kwa sauti: "Hakujapata kuwako mji kama mji huu mkuu!" |
19 | Wakajimwagia vumbi juu ya vichwa vyao wakilia kwa sauti na kuomboleza: "Ole! Ole kwako mji mkuu! Ni mji ambamo wote wenye meli zisafirizo baharini walitajirika kutokana na utajiri wake. Kwa muda wa saa moja tu umepoteza kila kitu!" |
20 | Furahi ee mbingu, kwa sababu ya uharibifu wake. Furahini watu wa Mungu, mitume na manabii! Kwa maana Mungu ameuhukumu kwa sababu ya mambo uliyowatenda ninyi! |
21 | Kisha malaika mmoja mwenye nguvu sana akainua jiwe mfano wa jiwe kubwa la kusagia, akalitupa baharini akisema, "Ndivyo, Babuloni atakavyotupwa na kupotea kabisa. |
22 | Sauti za vinubi za muziki, sauti za wapiga filimbi na tarumbeta hazitasikika tena ndani yako. Hakuna fundi wa namna yoyote ile atakayepatikana tena ndani yako; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikika tena ndani yako. |
23 | Mwanga wa taa hautaonekana tena ndani yako; sauti za bwana arusi na bibi arusi hazitasikika tena ndani yako. Wafanyabiashara wako walikuwa wakuu duniani, na kwa uchawi wako mataifa yote yalipotoshwa!" |
24 | Mji huo uliadhibiwa kwani humo mlipatikana damu ya manabii, damu ya watu wa Mungu na damu ya watu wote waliouawa duniani. |