Zaburi 11
Kumtumaini Bwana 
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. 
 1 Kwa Bwana ninakimbilia, 
unawezaje basi kuniambia: 
“Ruka kama ndege kwenye mlima wako. 
 2 Hebu tazama, waovu wanapinda pinde zao, 
huweka mishale kwenye uzi wake, 
wakiwa gizani ili kuwapiga 
wale wanyofu wa moyo. 
 3 Wakati misingi imeharibiwa, 
mwenye haki anaweza kufanya nini?” 
 4  Bwana yuko ndani ya Hekalu lake takatifu; 
Bwana yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni. 
Huwaangalia wana wa watu, 
macho yake yanawajaribu. 
 5  Bwana huwajaribu wenye haki, 
lakini waovu na wanaopenda jeuri, 
nafsi yake huwachukia. 
 6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali 
na kiberiti kinachowaka, 
upepo wenye joto kali ndio fungu lao. 
 7 Kwa kuwa Bwana ni mwenye haki, 
yeye hupenda haki. 
Wanyofu watauona uso wake.