Zaburi 12
Kuomba Msaada 
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi. 
 1  Bwana tusaidie, kwa kuwa wacha Mungu wametoweka; 
waaminifu wametoweka miongoni mwa wanadamu. 
 2 Kila mmoja humwambia jirani yake uongo; 
midomo yao ya hila huzungumza kwa udanganyifu. 
 3  Bwana na akatilie mbali midomo yote ya hila 
na kila ulimi uliojaa majivuno, 
 4 ule unaosema, “Kwa ndimi zetu tutashinda; 
midomo ni mali yetu, bwana wetu ni nani?” 
 5 “Kwa sababu ya uonevu wa wanyonge 
na kulia kwa uchungu kwa wahitaji, 
nitainuka sasa,” asema Bwana. 
“Nitawalinda kutokana na wale 
wenye nia mbaya juu yao.” 
 6 Maneno ya Bwana ni safi, 
kama fedha iliyosafishwa katika tanuru, 
iliyosafishwa mara saba. 
 7 Ee Bwana, utatuweka salama 
na kutulinda na kizazi hiki milele. 
 8 Watu waovu huenda wakiringa kila mahali 
wakati ambapo yule aliye mbaya sana 
ndiye anayeheshimiwa miongoni mwa watu.