Zaburi 13
Sala Ya Kuomba Msaada 
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. 
 1 Mpaka lini, Ee Bwana? Je, utanisahau milele? 
Utanificha uso wako mpaka lini? 
 2 Nitapambana na mawazo yangu mpaka lini, 
na kila siku kuwa na majonzi moyoni mwangu? 
Adui zangu watanishinda mpaka lini? 
 3 Nitazame, unijibu, Ee Bwana Mungu wangu. 
Yatie nuru macho yangu, 
ama sivyo nitalala usingizi wa mauti. 
 4 Adui yangu atasema, “Nimemshinda,” 
nao adui zangu watashangilia nitakapoanguka. 
 5 Lakini ninategemea upendo wako usiokoma; 
moyo wangu unashangilia katika wokovu wako. 
 6 Nitamwimbia Bwana, 
kwa kuwa amekuwa mwema kwangu.