Zaburi 14
Uovu Wa Wanadamu 
(Zaburi 53) 
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. 
 1 Mpumbavu anasema moyoni mwake, 
“Hakuna Mungu.” 
Wameharibika, matendo yao ni maovu kabisa; 
hakuna hata mmoja atendaye mema. 
 2  Bwana anawachungulia wanadamu chini 
kutoka mbinguni 
aone kama wako wenye akili, 
wowote wanaomtafuta Mungu. 
 3 Wote wamepotoka, 
wameharibika wote pamoja, 
hakuna atendaye mema. 
Naam, hakuna hata mmoja! 
 4 Je, watendao mabaya kamwe hawatajifunza: 
wale ambao huwala watu wangu 
kama watu walavyo mkate, 
hao ambao hawamwiti Bwana? 
 5 Wako hapo, wameingiwa na hofu kuu, 
maana Mungu yupo pamoja na wenye haki. 
 6 Ninyi watenda mabaya mnakwamisha mipango ya maskini, 
bali Bwana ndiye kimbilio lao. 
 7 Laiti wokovu wa Israeli 
ungalikuja kutoka Sayuni! 
Wakati Bwana arejeshapo 
wafungwa wa watu wake, 
Yakobo na ashangilie, 
Israeli na afurahi!