Zaburi 15
Kitu Mungu Anachotaka 
Zaburi ya Daudi. 
 1  Bwana, ni nani awezaye kukaa 
katika Hekalu lako? 
Nani awezaye kuishi 
katika mlima wako mtakatifu? 
 2 Ni yule aendaye pasipo mawaa, 
atendaye yaliyo haki, 
asemaye kweli toka moyoni mwake, 
 3 na hana masingizio ulimini mwake, 
asiyemtenda jirani yake vibaya, 
na asiyemsingizia mwenzake, 
 4 ambaye humdharau mtu mbaya, 
lakini huwaheshimu wale wamwogopao Bwana, 
yule atunzaye kiapo chake 
hata kama anaumia. 
 5 Yeye akopeshaye fedha yake bila riba, 
na hapokei rushwa dhidi ya mtu asiye na hatia. 
Mtu afanyaye haya 
kamwe hatatikisika.