Zaburi 16
Sala Ya Matumaini 
Utenzi wa Daudi. 
 1 Ee Mungu, uniweke salama, 
kwa maana kwako nimekimbilia. 
 2 Nilimwambia Bwana, “Wewe ndiwe Bwana wangu; 
pasipo wewe sina jambo jema.” 
 3 Kwa habari ya watakatifu walioko duniani, 
ndio walio wa fahari ambao ninapendezwa nao. 
 4 Huzuni itaongezeka kwa wale 
wanaokimbilia miungu mingine. 
Sitazimimina sadaka zao za damu 
au kutaja majina yao midomoni mwangu. 
 5  Bwana umeniwekea fungu langu na kikombe changu; 
umeyafanya mambo yangu yote yawe salama. 
 6 Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri, 
hakika nimepata urithi mzuri. 
 7 Nitamsifu Bwana ambaye hunishauri, 
hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha. 
 8 Nimemweka Bwana mbele yangu daima. 
Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume, 
sitatikisika. 
 9 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia; 
mwili wangu nao utapumzika salama, 
 10 kwa maana hutaniacha kaburini, 
wala hutamwacha Mtakatifu Wako kuona uharibifu. 
 11 Umenijulisha njia ya uzima; 
utanijaza na furaha mbele zako, 
pamoja na furaha za milele 
katika mkono wako wa kuume.