Zaburi 24
Mfalme Mkuu 
Zaburi ya Daudi. 
 1 Dunia ni mali ya Bwana, na vyote vilivyomo ndani yake, 
ulimwengu, na wote waishio ndani yake, 
 2 maana aliiwekea misingi yake baharini 
na kuifanya imara juu ya maji. 
 3 Nani awezaye kuupanda mlima wa Bwana? 
Ni nani awezaye kusimama patakatifu pake? 
 4 Ni yule mwenye mikono safi na moyo mweupe, 
yule ambaye hakuinulia sanamu nafsi yake 
au kuapa kwa kitu cha uongo. 
 5 Huyo atapokea baraka kutoka kwa Bwana, 
na hukumu ya haki kutoka kwa Mungu Mwokozi wake. 
 6 Hiki ndicho kizazi cha wale wamtafutao, 
wale wautafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. 
 7 Inueni vichwa vyenu, enyi malango, 
inukeni enyi milango ya kale, 
ili mfalme wa utukufu apate kuingia. 
 8 Ni nani huyu Mfalme wa utukufu? 
Ni Bwana aliye na nguvu na uweza, 
ni Bwana aliye hodari katika vita. 
 9 Inueni vichwa vyenu, enyi malango, 
viinueni juu enyi milango ya kale, 
ili Mfalme wa utukufu apate kuingia. 
 10 Ni nani yeye, huyu Mfalme wa utukufu? 
Ni Bwana Mwenye Nguvu Zote; 
yeye ndiye Mfalme wa utukufu.