Zaburi 28
Kuomba Msaada 
Zaburi ya Daudi. 
 1 Ninakuita wewe, Ee Bwana, Mwamba wangu; 
usiwe kwangu kama kiziwi. 
Kwa sababu ukinyamaza 
nitafanana na walioshuka shimoni. 
 2 Sikia kilio changu unihurumie 
ninapokuita kwa ajili ya msaada, 
niinuapo mikono yangu kuelekea 
Patakatifu pa Patakatifu pako. 
 3 Usiniburute pamoja na waovu, 
pamoja na hao watendao mabaya, 
ambao huzungumza na jirani zao maneno mazuri, 
lakini mioyoni mwao wameficha chuki. 
 4 Walipe sawasawa na matendo yao, 
sawasawa na matendo yao maovu; 
walipe sawasawa na kazi za mikono yao, 
uwalipe wanavyostahili. 
 5 Kwa kuwa hawaheshimu kazi za Bwana, 
na yale ambayo mikono yake imetenda, 
atawabomoa na kamwe 
hatawajenga tena. 
 6  Bwana asifiwe, 
kwa maana amesikia kilio changu 
nikimwomba anihurumie. 
 7  Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu, 
moyo wangu umemtumaini yeye, 
nami nimesaidiwa. 
Moyo wangu unarukaruka kwa furaha 
nami nitamshukuru kwa wimbo. 
 8  Bwana ni nguvu ya watu wake, 
ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake. 
 9 Waokoe watu wako na uubariki urithi wako; 
uwe mchungaji wao na uwabebe milele.