Zaburi 29
Sauti Ya Bwana Wakati Wa Dhoruba 
Zaburi ya Daudi. 
 1 Mpeni Bwana, enyi mashujaa, 
mpeni Bwana utukufu na nguvu. 
 2 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake; 
mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake. 
 3 Sauti ya Bwana iko juu ya maji; 
Mungu wa utukufu hupiga radi, 
Bwana hupiga radi juu ya maji makuu. 
 4 Sauti ya Bwana ina nguvu; 
sauti ya Bwana ni tukufu. 
 5 Sauti ya Bwana huvunja mierezi; 
Bwana huvunja vipande vipande 
mierezi ya Lebanoni. 
 6 Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama, 
Sirioni* Yaani Mlima Hermoni. urukaruke kama mwana nyati. 
 7 Sauti ya Bwana hupiga kwa miali 
ya umeme wa radi. 
 8 Sauti ya Bwana hutikisa jangwa; 
Bwana hutikisa Jangwa la Kadeshi. 
 9 Sauti ya Bwana huzalisha ayala, 
na huuacha msitu wazi. 
Hekaluni mwake wote wasema, 
“Utukufu!” 
 10  Bwana huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika; 
Bwana ametawazwa kuwa Mfalme milele. 
 11  Bwana huwapa watu wake nguvu; 
Bwana huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.